MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imesema Mkoa wa Kilimanjaro ulipata mvua kubwa usiku wa kuamkia jana kuliko mikoa yote kwa kupata milimita 78.7 huku Mkoa wa Dar es Salaam ukipata milimita 24.7.
Mtaalamu wa hali ya hewa kutoka TMA, Rose Senyagwa alisema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLEO kuhusu mvua za masika zinazoendelea kunyesha nchini.
Alisema mvua hizo za masika zimeendelea kunyesha kwenye maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Pwani wa Kaskazini na Ukanda wa Ziwa Victoria.
"Matarajio wiki ya kwanza Aprili mvua zitaendelea kuwapo. Upungufu wa mvua unatarajiwa mwisho wa wiki ya kwanza na ya pili ya Aprili," alisema.
Aliongeza kuwa mvua zinatarajiwa kuwepo tena katika wiki ya tatu na nne ya Aprili.
"Kumekuwepo na ongezeko la joto hususani wiki tatu za Machi kutokana na upungufu wa mvua. Tunatarajia Aprili joto litapungua kutokana na uwepo wa mvua," alisema.
Juzi TMA ilitoa ufafanuzi wa sababu ya kuchelewa kunyesha mvua kwa baadhi ya maeneo licha ya mvua hizo kutarajiwa kuanza kunyesha wiki ya tatu na ya nne ya Februari.
Ilisema licha ya mvua hizo kuanza kunyesha kama ilivyotarajiwa Februari bado kumetokea vipindi virefu vya ukavu kuanzia wiki ya kwanza ya Machi hususani kwa baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na Ukanda wa Pwani ya Kaskazini Mashariki.
TMA ilisema hali hiyo ilisababishwa na uwepo wa vimbunga hasa kimbunga Gombe kilichodumu kwa muda mrefu katika Bahari ya Hindi eneo la rasi ya Msumbiji.