Fahamu zaidi kuhusu tatizo la ugonjwa wa Polio

 


Polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vinavyoingia mwilini kupitia mdomoni kwa njia ya kula chakula au kunywa kinywaji. Virusi hivyo hupatikana kwenye kinyesi cha binadamu ambacho huwa na virusi vya ugonjwa wa polio ambapo kinyesi hicho kikiingia kwenye maji na yakatumiwa na mtu kwa njia ya kupikia chakula au kunywa huweza kuambukizwa ugonjwa huo.


Takriban asilimia 90 hadi 95 ya wanaoambukizwa ugonjwa huu huwa hawaoneshi dalili zozote, huku asilimia 5 hadi 10 ya watu huonesha dalili hafifu za homa, maumivu ya kichwa, kutapika, kuharisha, mishipa ya shingo kukaza na maumivu katika miguu na mikono.


Hali hiyo hutokana na virusi hivyo vinapofika kwenye tumbo huweza kusafiri hadi kwenye ubongo na uti wa mgongo ambapo mgonjwa huweza kuhisi maumivu ya kichwa, kukakamaa kwa shingo pamoja na maumivu ya miguu na mikono.


Kwa kawaida watu hawa hurejea katika hali ya kawaida baada ya wiki moja au mbili. Asilimia 0.5 ya waathrika huweza kupata udhaifu wa misuli suala linalosababisha kushindwa kutembea. Hali hiyo huweza kutokea katika masaa kadhaa baada ya maambukizo.


Virusi vya polio vinapofika tumboni huweza kuzaliana na kuongezeka, hivyo kuanza kushambulia neva na kusababisha mgonjwa kupooza baadhi ya viungo. Ugonjwa huu, huwapata zaidi watoto walio chini ya umri wa miaka miwili kuliko wale ambao wameshavuka umri huo.


Ingawa ni asilimia ndogo sana ya wanaopatwa na polio huweza kupata ulemavu wa mwili wa kudumu, lakini hatari hiyo inalazimu ugonjwa huo kupewa umuhimu mkubwa na kuzuiwa kupitia chanjo.


Ugonjwa wa polio unaweza kuzuilika kupitia chanjo, hata hivyo dozi kadhaa hutakiwa ili chanjo iweze kuwa na athari. Pale mtu anapopatwa na ugonjwa huu huwa hakuna dawa maalumu ya kumtibu. Mwaka 2013 polio iliwaathiri watu 416 duniani ikilinganishwa na mwaka 1988 ambapo watu laki na nusu walipatwa na ugonjwa huu.


Mafanikio hayo yametokana na kupewa umuhimu chanjo kwa watoto takribani katika maeneo yote duniani suala lililoleta matumaini ya kutokomezwa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2018. Lakini mwaka huu wa 2014 ugonjwa wa polio ulishuhudiwa katika nchi za Afghanistan, Nigeria na Pakistan.


Ni zipi dalili za ugonjwa wa polio? Mtu mwenye ugonjwa huo hupata dalili za kuumwa na kichwa, shingo kukakamaa mwili na miguu na mikono kuwa na maumivu. Zipo dalili nyingine ambazo hazionekani mara kwa mara ambazo kupelekea baadhi ya viungo kulegea au kupooza.


Ugonjwa huu unaweza kuathiri sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo mikono, miguu na sehemu nyinginezo. Aidha baadhi ya watu wanaweza kuathirika kuanzia maeneo ya nyonga kushuka chini jambo linalopelekea kukosa mawasiliano kati ya sehemu hizo mbili hata kupelekea kushindwa kudhibiti haja kubwa na ndogo. Zile sehemu zinazokuwa zimeathirika zinaweza kupata nafuu pale mgonjwa atakapokuwa anafanya mazoezi ya viungo kwa kiasi kinachotakiwa.


Kinga na matibabu yake

Ugonjwa wa polio kwa bahati nzuri unaweza kuzuilika kwa kupata chanjo hasa kwa watoto wadogo chini ya miaka miwili. Chanjo ndio njia pekee ya kupambana na ugonjwa huu ambao una madhara hasa ya kusababisha ulemavu na hata kumfanya mtu awe tegemezi maishani.


Chanjo hizo huweza kutolewa kwa watoto kuanzia miezi miwili ambapo hupewa dawa kwa njia ya matone na sindano. Hata hivyo watoto na watu wazima waliopata chanjo ya kuzuia polio wanaweza kupata ugonjwa huo tena ingawa unakuwa hauna makali sana ukilinganisha na yule ambaye hajapata chanjo hiyo.


Aidha kwa wale ambao wamepatwa na ugonjwa huu hakuna dawa ya kuweza kutibu ugonjwa huo zaidi ya matibabu kwa njia ya mazoezi. Kwa kawaida ni vigumu kutibu mtu aliyepooza zaidi ya kumpatia dawa ya kupunguza maumivu kwani hakuna dawa itakayoweza kuondoa kupooza. Kutokana na ugonjwa huu kukosa tiba chanjo, watu wanatakiwa kuchukua tahathari kubwa hasa wale wenye kuwahudumia wagonjwa wa polio.


Watu wanaowahudumia wagonjwa wa polio wanatakiwa kuzingatia zaidi usafi pale wanapomaliza kuwahudumia wagonjwa hao kwani wanaweza kujisahau na kula kitu jambo linaloweza kuwapatia maambukizi ya ugonjwa huo.


Pia ni muhimu wazazi na walezi kuhakikisha mtoto amepata matone akiwa na umri wa miezi miwili, mitatu na minne. Pia hata wale ambao waliwahi kuugua ugonjwa huo na kupona, wanaweza kuugua tena kwa mara ya pili ingawa sio wote. Inashauriwa kuwa mtoto au mtu mzima aliyepata ugonjwa huo na kupooza ale chakula bora pamoja na kufanya mazoezi ili kuipa nguvu misuli iliyobaki mwilini bila kuathirika.

Katika mazoezi hayo anatakiwa kufuata ushauri wa daktari ili kuweza kufanya mazoezi kadiri inavyotakiwa kwani iwapo atazidisha mazoezi anaweza pia kupata madhara. Kama amepata matatizo kwenye miguu anatakiwa kusaidiwa kutembea kadri anavyoweza na baada ya muda apatiwe msaada wa kutembea kama vile kutafutiwa magongo ya kutembelea.


Aidha kwa watu waliowahi kuugua ugonjwa huo wanaweza kuwa na matatizo ya kupumua yanayosababishwa na ugonjwa huo kudhohofisha misuli ya kupumua hivyo wanaposhindwa kupumua wanatakiwa kusaidiwa kupumua kwa njia yoyote ikiwemo ya kuwaweka kwenye mashine za kupumulia.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad