Baraza la Seneti nchini Marekani limepiga kura kuendelea na mchakato wa mashitaka dhidi ya rais wa zamani Donald Trump, likisema mchakato huo ni wa kikatiba.
Baraza la Seneti lilipiga kura 56 kwa 44 za kuendelea na kesi dhidi ya Trump, likizipinga hoja za mawakili wake kwamba rais hawezi kushitakiwa pindi anapomaliza muda wake.
Maseneta ambao waliapishwa kama wazee wa baraza, walipitia picha za vidio za wafuasi wa Trump wakipambana na polisi, kuvamia kumbi za bunge na kupeperusha bendera za Trump. Pia kuliwasilishwa vidio za Trump mwenyewe akiwahimiza wafuasi wake kabla ya uvamizi kuwa wapambane hadi tone la mwisho kupinga kushindwa kwake kwenye uchaguzi wa Novemba 3.
Kiongozi mkuu wa mashitaka hayo Jammie Raskin aliwaeleza maseneta kwamba kesi hiyo itawasilisha “ukweli mgumu” dhidi ya Trump. “Rais Trump ametuma mawakili wake hapa leo kujaribu kuzuia Bunge la Seneti kusikia ukweli wa kesi hii. Wanataka kuzima kesi kabla hata ya ushahidi wowote kutolewa. Hoja yao ni kwamba ikiwa unafanya makosa ya kushitakiwa katika wiki zako za mwisho mamlakani, basi unafanya ukiwa na kinga ya kikatiba na unanusurika”.
Mawakili wa Trump wameendelea kuushambulia mchakato huo wakisema ni kinyume na katiba na kwamba ni juhudi za kumzuia kiongozi huyo kuwania tena nafasi ya urais. Wakili anayeongoza jopo la utetezi upande wa Trump Bruce Castor, amesema mashitaka dhidi ya rais huyo hayahitajiki tena kutokana na kwamba kiongozi huyo aliondolewa madarakani kupitia kura na hivyo lengo la kikatiba tayari limefanikiwa.
Trump anakabiliwa na shtaka moja la uchochezi wa uasi baada ya wafuasi wake kuvamia majengo ya bunge mnamo mwezi Januari. Alishitakiwa na baraza la wawakilishi Januari 13.
Maseneta wengi wa Republican wameashiria kuwa hawatopiga kura ya kumtia hatiani Trump na hivyo kuna uwezekano akavuka kiunzi hicho. Ili aweze kukutwa na hatia kunahitajika theluthi mbili ya wingi wa kura kwa maana kwamba angalau maseneta 17 wa Republican itabidi wajiunge na wenzao 48 wa Democatrs katika kupiga kura dhidi ya Trump ambaye amesalia kuwa mtu aliye na nguvu ndani ya chama chake licha ya kuondoka mamlakani.
Trump ni rais pekee kushitakiwa katika baraza la seneti baada ya kumaliza muda wake madarakani na wa kwanza kushitakiwa mara mbili. Mchakato huo unaendelea leo chini ya ulinzi mkali katika maeneo yote ya bunge.