Harmonize: Mwana Kulitafuta, Mwana Kulipata




MWANA kulitafuta, mwana kulipata! Ndiyo kauli inayomfaa staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ Harmonize ambaye ametoa hoja ambayo imekutana na upinzani mkubwa na kujikuta akishambuliwa kwa maneno makali na matusi.

 

Harmonize amekuwa na hoja yake kwa muda mrefu akiwataka wasanii wenzake kufikiria njia mpya ya kukuza na kuufikisha mbali muziki wa Bongo Fleva.



Kwa nyakati tofauti, Harmonize amesikika kwenye intavyu zake mbalimbali akitamba kuwa ana kipaji kikubwa ambacho ni lazima kiifikie Dunia nzima!

 

Mwenyewe anaamini kwamba ili lengo lake hilo alifikie, basi ni lazima wasanii wenzake wamuige katika matumizi ya lugha ya Kingereza kwenye utuzi na uimbaji wa ngoma zao.

 

Harmonize anaamini kwamba Kiswahili kimetumiwa kwa muda mrefu kwenye muziki na kukubalika kwa miaka mingi, lakini sasa ni muda muafaka kwa wasanii kuangalia namna nyingine ya kupanua muziki wa Bongo Fleva kufikia watu wengi zaidi duniani hivyo kuuza zaidi.

 

Harmonize anatoa mfano wa ngoma zake mbili za Bedroom na Fall In Love ambazo zimefanya vizuri mno kwa kuwa ametumia lugha ya Kingereza kuandika mashairi na kuimba.

 

Kwenye ngoma yake mpya ya All Night aliyomshirikisha msanii mpya aitwaye Anjella tayari ngoma hiyo imekwenda mbali mno na kuweka rekodi kwenye mitandao ya kusikiliza na kutazama muziki kwa sababu ametumia lugha ya Kingereza!



“Nina wajibu wa kuwashukuru sana waanzilishi wa muziki huu ambao leo umekuwa ni ajira kwetu na unasaidia familia zetu za kimaskini, lakini pia wadau na mashabiki kwa kupambana mpaka tasnia ilipofia hapa.“Kiukweli haikuwa rahisi, lakini pia niseme sanaa yetu imekuwa kubwa mataifa kibao wanafuata tunachofanya ni ishara tosha kwamba tunapiga bao.

 

“Ila nina kaujumbe kafupi tu, nadhani ni time (muda) sasa wa kuutangaza muziki pamoja na Tanzania mbali zaidi, tumekuwa tukiitangaza lugha yetu pendwa kwa muda mwingi mno na kuifanya imekuwa lugha maarufu sana Afrika…!

 

“Ni Kiswahili, lakini nadhani ni wakati muafaka wa kuutangaza muziki wetu pamoja na nchi yetu…”Katika hoja hiyo tumekuwa tukishuhudia baadhi ya wasanii kama Mbosso ambaye amekuwa akitafsiri mashairi yake ya Kiswahili kwenda kwenye Kingereza ambapo ukitazama video zake utayaona yakipita chini ya skrini.Katika kuonesha msisitizo juu ya hilo, Harmonize aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram;

 

“Njia rahisi ni kuimba muziki wa Kitanzania naku-shoot video Tanzania, ila wimbo unaimba kwa lugha ambayo Dunia nzima inaelewa..!!!! Nayo ni English (Kingereza).“Ndugu wasanii msiwe na wasiwasi tuondoeni zile dhana za zamani eti ukiimba kizungu ngoma haiwezi ku-hit.



“Watanzania wa leo siyo wa jana karibia wote wanatema mayai (kuongea Kingereza).“Mmeona mifano kama Bedroom na Falling In Love; hizi zote ni hit (ni ngoma zilizokubalika) na zimeimbwa kwa English (Kingereza). Japokuwa ukitia vineno viwili-vitatu vya lugha yetu mama siyo mbaya…..!!!!

 

”Hata hivyo, wakati Harmonize akiamini kwamba Kingereza kitasaidia kuuza muziki wake duniani kote, baadhi ya mashabiki wake hawakubaliani naye na wamekuwa na maoni tofauti kabisa huku wengine wakimshambulia kwa maneno makali kwamba analewa umaarufu na kuanza kuidharau lugha ya Taifa lake ya Kiswahili.

 

Mashabiki wengi waliomshambulia Harmonize kwa hoja yake hiyo, wameibuka na hoja kuwa muziki hautambulishwi kwa lugha. Wanatolea mfano Ngoma ya Despacito ya Luis Fonsi ambayo imesikilizwa na kutazamwa mara zaidi ya bilioni saba; sawa na idadi ya watu wote duniani wakati imeimbwa kwa Lugha ya Kihispaniola.

 

Baadhi yao wanamjibu Harmonize kuwa, hata ngoma za Kiswahili za aliyekuwa bosi wake kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, zimekuwa ngoma za Dunia na ushahidi wa hilo upo wazi kwa kuzama kwenye YouTube namba ambavyo zina watazamaji na wasikilizaji wengi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad