Ijue Hatari ya Matumizi Holela ya Dawa ya Kuzuia Mimba P2

Dar es Salaam. Ujana ni maji ya moto. Ni msemo maarufu ukiwalenga vijana wakiwamo wasichana ambao ujana wao unawasukuma kujiunguza kwa ‘maji ya moto’.


Hata hivyo kwa muktadha wa habari hii, maji haya ni kitendo wanachokifanya wasichana hao kutumia njia mbalimbali hata zisizo salama ili kuzuia mimba.


Miongoni mwa njia zinazotumiwa ni matumizi ya vidonge vya ‘Emergence Contraceptive Pills’ maarufu kama P2. inaelezwa kuwa wasichana wamekuwa wakivimeza baada ya kufanya ngono zembe kama njia ya kuzuia ujauzito.


Ingawa kitaalamu P2 zinashauriwa zimezwe saa 48 hadi 72 baada ya tendo ili kuzuia mimba kutungwa, wasichana wengi inadaiwa wamekuwa wakitumia dawa hizo kiholela bila kufuata ushauri wa daktari.


Kwa mujibu wa taratibu za nchi za kitatibu na kifamasia, P2 kama ilivyo kwa dawa nyingine zinatakiwa kutolewa kwa maelekezo ya daktari .


Akizungumza na Mwananchi jana, Msajili wa Baraza la Famasia nchini, Elizabeth Shekalaghe alisema P2 ni dawa ambayo inaruhusiwa kuuzwa katika katika maduka ya dawa kwa maelekezo ya cheti cha daktari.


ADVERTISEMENT

“Ni dawa ya cheti, lazima mnunuzi aonyeshe cheti cha daktari ndipo itolewe na duka la dawa linatakiwa kuuza dawa mbalimbali zilizoruhusiwa ikiwamo hiyo isipokuwa baadhi ya dawa zikiwamo za HIV na zilizopo katika mpango wa Serikali,” alifafanua Shekalaghe.


Meneja wa huduma za sheria kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA), Wakili Iskari Fute alisema kwa mujibu wa kanuni ya makundi ya dawa yenye masharti mbalimbali ya matumizi, dawa hiyo itatumiwa kwa masharti ambayo TMDA imeyaweka.


“Kwa mujibu wa kanuni ya masharti ya matumizi ya dawa ya mwaka 2015, P2 ni dawa ambayo lazima itolewe kwa cheti cha daktari,” alibainisha Wakili Fute.


Mwanamke mmoja aitwaye Betty ((si jina halisi) aliiambia Mwananchi kuwa ameshatumia P2 mara nyingi katika kipindi cha miaka minne.


“Sijawahi kushauriwa na daktari bali rafiki zangu, nimekuwa natumia mara mbili kwa miezi mitatu,” aliongeza Betty.


Muuzaji mmoja wa duka moja la dawa kubwa lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam, Juma Abdalla alisema dawa hiyo hununuliwa zaidi na wasichana wa rika la miaka 14 mpaka 30 ambao wengi hufika wakihitaji dozi zaidi ya moja.


“Huwa tunawashauri kwamba waeleze tatizo lakini wengi hawapendi na wanataka wauziwe waondoke. Mara kadhaa tumekuwa tukikataa kutoa ingawa dawa hizi tunaziuza sana ikilinganishwa na dawa nyingine na mara nyingine wanaume huja kununua,” anasema muuzaji huyo.


Hata hivyo baadhi ya maduka yalikiri kuuza kwa wingi vidonge hivyo hasa yale yaliyopo maeneo ya Posta, Makumbusho, Mlimani City na Survey jijini Dar es Salaam.


Onyo la wataalamu


Hata hivyo, wataalamu wanaonya matumizi ya dawa hizo kuwa zina madhara zisipotumiwa kwa kufuata maelekezo.


“Unapozungumzia P2 unaongelea vidonge vya kuzuia mimba kwa hiyo anayeshauriwa kutumia ni yule ambaye imetokea kweli bahati mbaya amekutana na mwenzake bila kujua kwamba ni kipindi cha hatari,” alisema daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Living Colman.


Dk Colman alisema haishauriwi kutumia dawa hiyo mara nyingi kwani husababisha mlundikano wa uzazi wa mpango katika mfumo wa kizazi ambao una madhara baadaye.


“Anayetumia mara kwa mara ina maana kwamba anajiwekea homoni nyingi mwilini ambazo baadaye zinaweza kuvuruga mfumo wa uzazi na pengine akashindwa kupata mtoto,” alionya Dk Colman.


Mfamasia na mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Muhimbili (Muhas) David Myemba alisema matumizi ya dawa ambazo zinamezwa kiholela hasa za kuzuia mimba au zile za kutibu matatizo yanayohusiana na hedhi, hali hiyo hutengeneza tatizo.


“Dawa hizi mara nyingine huwa zinaenda mpaka kwenye mfumo wa damu na wakati mwingine husababisha kiharusi na hata tatizo la moyo na magonjwa mengine,” alitahadharisha.


Myemba alisema kwenye mfumo wa kizazi dawa zinazotumika kuzuia mimba zina matokeo hasi zikitumika kwa muda mrefu.


“Shida inakuja imeshakuwa kama tabia kwa mabinti wengi wenye umri mdogo wanapenda kuzitumia, na kujiletea madhara,” aliongeza Myemba.


Aliongeza kusema kuwa madhara yake mengine ni kusababisha saratani ya matiti na kuonya matatizo ya dawa hizo huwa hayaonekani mara moja.


Myemba alisema pia utumiaji holela wa vidonge vya P2 husababisha mabadiliko ya mzunguko wa hedhi kwa wengi.


“Huleta shida katika mzunguko wa siku za hedhi, pia kuna presha kushuka na wakati mwingine mhusika huenda akapoteza damu nyingi wakati wa hedhi au akapata kidogo sana wakati mwingine unaweza pata hedhi siku ambazo si kawaida, kama alienda siku tatu ataenda sita kama ilikuwa siku tano akaanza kupata siku mbili,” aliongeza Myemba.


Alitaja madhara mengine kuwa ni kuongezeka uzito na wakati mwingine mifupa inakuwa dhaifu.


 

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad