RAIS John Magufuli amepandisha cheo Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Zephrine Galeba, aliyeandika hukumu kwa lugha ya Kiswahili na sasa anakuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa.
Magufuli ametoa uamuzi huo leo Jumatatu, Februari 1, 2020, wakati akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama Kuu.
“Nilipoingia madarakani niliambiwa sijui Kiingereza wala sikujali, UDSM (Chuo Kikuu cha Dar es Sakaan) nimekaa miaka mitatu nikisoma masomo yangu ya sayansi, na nikakaa mwaka mzima Uingereza sijui nilikuwa nazungumza Kisukuma kule! Niliamua kuzungumza Kiswahili lengo ni kuki-promote (kukiendeleza).
“Sasa wakati umefika wa kuanza kuweka mikakati ya lugha ya Kiswahili kutumika katika masuala ya kimahakama na kisheria katika ngazi zote, Kiswahili kinatumika AU (Umoja wa nchi za Afrika), SADC (JUmuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika) , EAC (Jumuia ya Afrika Mashariki), n.k, sioni sababu ya kwa nini mahakama hamtaki kutumia Kiswahili, kushindwa kutumia lugha hii siyo tu tunawanyima haki wananchi bali tunawaongezea gharama kupitia ukalimani wa kutafsiri hukumu na mienendo ya kesi.
“Jaji Mkuu hapa umezungumza Kiswahili kizuri kuliko changu cha Kisukuma, lakini ukienda kuhukumu unaandika Kiingereza, hicho Kiswahili kimepotelea wapi? Hii ni changamoto kubwa, lazima tubadilike na tukipende kilicho chetu.
“Ukimwandikia hukumu mtu kule kijijini Katahoka, Biharamulo, hukumu imeandikwa kwa Kiingereza yule bibi kizee wa kijijini kule aende akatafute wa kutafsiri ‘amesemaje hapa?’ Tunatengeneza kero kwa Wwnanchi, kuandika hukumu kwa Kiswahili sio dhambi.
“Hii ya kuandika hukumu kwa Kiingereza inatia dosari kwenye uhuru tulionao, nampongeza Jaji Gareba wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma kwa kutumia Kiswahili katika kutoa hukumu ya North Mara Gold Mining dhidi ya Gerald Zumbi katika kesi ya mapitio No.23 ya mwaka 2020.
“Najua alisemwa semwa sana, nakushukuru Jaji Mkuu hamkumpa adhabu, amekuwa mzalendo wa kwanza kuandika hukumu kwa Kiswahili, nampongeza, huyu ni shujaa wa Kiswahili katika mahakama, nampandisha cheo kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa,” amesema Magufuli.