KOCHA Mkuu wa Yanga Mrundi Cedric Kaze amefanya kikao na mshambuliaji wake Abdoul Razak Fiston na kumwambia asisikilize presha ya mashabiki na badala yake afanye kazi yake iliyomleta ya kufunga mabao.
Hiyo ni baada ya mshambuliaji huyo kucheza mchezo wake wa kwanza wa kirafiki dhidi ya African Sports uliopigwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam na matokeo kumalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0, mchezo ambao alionyesha kiwango cha chini.
Katika mchezo huo, kocha huyo alikitumia nusu ya kikosi kilichobeba Kombe la Mapinduzi lililofanyika mwezi uliopita huko visiwani Zanzibar.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kaze alisema kuwa anaamini uwezo mkubwa alionao Fiston na kikubwa mashabiki wawe na imani naye katika michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara.
Kaze alisema kuwa amekaa kikao na staa huyo na kikubwa amemtaka kupunguza presha anapofika katika eneo la kufunga mabao ndani na nje ya 18 ili kuhakikisha anakata kiu ya mashabiki wa Yanga.
Aliongeza kuwa katika kikao chake mshambuliaji huyo ameahidi kufanyia kazi maelekezo na ushauri wote aliopewa kwa kuanza ataanza na mchezo wa ligi dhidi ya Mbeya City utakaoupigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
“Sina hofu na kiwango cha mshambuliaji wangu mpya Fiston kwani anahitaji muda zaidi, kingine ana muda mrefu hakucheza soka.“Ni vigumu kuonekana ubora wake kwenye mchezo mmoja nadhani ni hali inayowakuta wachezaji wengi, kikubwa ninachoweza kusema atakuwa msaada mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji.“
Mchezo wetu dhidi ya African Sports ambao ulikuwa wa kirafiki, wachezaji wangu walikuwa kwenye wiki mbili ngumu za kufanya mazoezi makali na mchezo huu ulikuwa maalum kutengeneza utimamu wa miili yao.
“Hivyo sioni kama kuna tatizo kwa kuwa tumetengeneza nafasi nyingi tulikosa bahati ya kutumia nafasi hizo, lakini kwangu kipimo changu ni kuwaona kama mafundisho niliyowapa wamefanyia kazi akiwemo Fiston ambaye nimekaa naye na kuzungumzia mechi hiyo,” alisema Kaze.
Stori: Wilbert Molandi naMusa Mateja, Dar