KOCHA Mkuu wa Yanga, Mrundi Cedric Kaze amesema kuwa kuna uwezekano wa kuwachezesha kwa pamoja viungo wake Carlos Carlinhos na Saido Ntibazonkiza kulingana na aina ya wapinzani atakaokutana nao.
Carlinhos na Saido hawajawahi kucheza kwa pamoja katika mchezo wowote wa ligi hiyo kutokana na majeraha aliyopata Carlinhos na kusababisha awe nje ya uwanja huku Saido akiwa anacheza.
Akizungumza na Championi Jumamosi Kocha Kaze alisema kuwa kuna uwezekano wa kuwatumia kwa pamoja wachezaji hao kulingana na aina ya mchezo husika kwani anaamini ni wachezaji wenye viwango vikubwa kutokana na uwezo wao wa kufunga pamoja na kutengeneza nafasi.
“Carlinhos na Saido ni wachezaji wazuri wenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao na kutengeneza pia, kuhusu kuwachezesha kwa pamoja inawezekana kwa kuwa wote wanaweza kucheza kutokea pembeni na katikati, hivyo kama mmoja atacheza kati basi mwingine ataanzia pembeni.
“Yote hiyo inatokana na aina ya wapinzani ambao tutakutana nao, kuna mechi nyingine huwezi kuwatumia wote itabidi umtumie mmoja na mwingine asubiri, kikubwa kwa sasa nafurahi kuona wote ni wazima,” alisema kocha huyo