CEDRIC KAZE, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa wale wanaoibeza kazi yake waendelee kufanya hivyo kwa kuwa yeye anajua kile anachokifanya na kushindwa kupata matokeo kumemfanya atambue tabia halisi za Watazania.
Kwenye mechi zake mbili mfululizo za mzunguko wa pili, Kaze alikiongoza kikosi hicho kwa kuambulia pointi mbili wakati alipokuwa akisaka pointi sita na kushuhudia nyavu zake zikiguswa mara nne sawa na idadi ya mabao ambayo alifunga.
Alianza na sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Mbeya City, Uwanja wa Sokoine Mbeya, aliporejea Dar akakutana na sare ya kufungana mabao 3-3 dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Mkapa.
Mchezo wake wa tatu alishinda bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa kwa bao la Carlos Carlinhos.
Kaze amesema: “Sikuwa kwenye wakati mzuri hasa baada ya kutopata matokeo mazuri ndani ya uwanja na jambo hilo lilinifanya nijue tabia za Watanzania kwa kuwa wengi wanapenda kuongea.
“Labda niseme kwamba ikiwa utanibeza uwezo wangu mimi sawa kwa kuwa ninajua ninachokifanya ila sikuwa kwenye wakati mzuri wakati wa matokeo haya mabaya. Nimeona kuna watu wanajiita wachambuzi walikuwa wanasema kwamba nimeishiwa mbinu, sijui nini na nini, mambo mengi kweli wameongea.”