Wanaakiolojia nchini Misri wamegundua kile kinachodaiwa kuwa kiwanda cha zamani zaidi cha bia ulimwenguni, kilichojengwa miaka 5,000 iliyopita.
Jopo la wanaakiolojia wa Misri na Marekani liligundua kiwanda hicho katika eneo la Abydos, lenye makaburi ya kale jangwani.
Walipata vitengo kadhaa vyenye sufuria zipatazo 40 zilizotumiwa kupasha mchanganyiko wa nafaka na maji kutengeneza pombe.
Kiwanda hicho huenda kilijengwa enzi ya Mfalme Narmer, kwa mujibu wa Baraza Kuu la Mambo ya Kale.
Baraza hilo linaamini "kuwa ni kiwanda kikongwe cha uzalishaji wa juu zaidi wa pombe ulimwenguni".
Mfalme Narmer aliongoza zaidi ya miaka 5,000 iliyopita. Alianzisha Nasaba ya Kwanza na inafahamika kuwa aliunganisha Misri.
Kiwanda hicho kilikuwa na maeneo makubwa manane, yaliyo na urefu wa mita 20 (65ft) na kila moja ikiwa na sufuria za udongo 40 zilizopangwa kwa safu mbili, kulingana na katibu mkuu wa Baraza Kuu la Mambo ya Kale nchini Misri, Mostafa Waziry.
Mchanganyiko wa nafaka na maji iliyotumiwa kutengeneza pombe ulichemshwa, kila sufuria "iliyoshikiliwa na viboreshaji vilivyotengenezwa kwa udongo vilivyowekwa wima kwa njia ya pete ", anasema.
Kiwanda hicho "huenda kilijengwa katika eneo hilo kwa lengo la kuendeleza matambiko ya kifalme yaliyokuwa yakifanyika ndani ya ukumbi huo wa makaburi ya wafalme wa Misri ", taarifa ya Wizara ya Utalii ya Misri ilimnukuu mwanaakiolojia mwenza Matthew Adams wa Chuo Kikuu cha New York.
Bia ilidhaniwa kutengenezwa kwa kiwango kikubwa, huku karibu lita 22,400 sawa na (mitungi 5,000) ikitengezwa wakati mwingine.
"Ushahidi wa kutumiwa kwa bia kufanya matambiko uligunduliwa wakati eneo hili lilipochimbwa,"taarifa hiyo ilisema.
Abydos ni moja ua miji mikongwe ya Misri ya kale yenye makaburi ya zamani na mahekalu.
Eneo hilo ambalo liko katika mkoa wa kusini wa Sohag, nchini Misri, pia lina miji wa Luxor, moja ya sehemu maarufu inayopendwa na watalii.
Mapema mwezi huu, wanaakiolojia walifukua mabaki ya watu wa kale wenye miaka 2,000 wakiwa na ndimi za rangi ya dhahabu Kaskazini mwa Misri.