DIDIER Gomes, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa mabao ambayo walifungwa jana Uwanja wa Mkapa yote yalikuwa mazuri jambo ambalo lilimfanya mlinda mlango Aishi Manula asiwe na chaguo.
Pia safu yake ya ulinzi chini ya Pascal Wawa na Ibrahim Ame haikuwa na chaguo la kufanya kuzuia safu ya ushambuliaji ya Azam FC kuweka mzani sawa kipindi cha pili.
Simba ilikubali sare ya kufungana mabao 2-2 na kugawana pointi mojamoja jambo lililowafanya waachwe kwa jumla ya pointi tano na watani zao wa jadi, Yanga ambao ni vinaara wakiwa na pointi 44.
Bao la Meddie Kagere kipindi cha kwanza liliwekwa usawa na Idd Seleman,'Naldo' kipindi cha pili kwa shuti kali akiwa nje ya 18 na bao la pili lilifungwa na Ayoub Lyanga kwa shuti akiwa ndani ya 18 huku Luis Miquissone akiweka usawa kwa Simba.
Gomes amesema:"Siwezi kuwalaumu mabeki wangu wala kipa kwa kilichotokea kwa kuwa yalikuwa mabao ya mbinu na mazuri hasa kwa wapinzani wetu hivyo ni darasa kwetu kuwa makini kwenye mechi zetu zijazo.
"Kikubwa ni kuona kwamba tunakuwa imara kwenye mechi zetu zijazo na kupata matokeo mazuri kwani mchezo umekwishwa na matokeo hayawezi kubadilika," .
Sare hiyo inawafanya Simba wafikishe jumla ya pointi 39 wakiwa nafasi ya pili huku Azam FC ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake ni 33.