Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kagera imewafikisha mahakamani watumishi wanne wa kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Stamigold kwa tuhuma za kuisababishia hasara ya Sh1.1 bilioni.
Walifikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Biharamulo Februari 12, 2021 wakidaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na kutumia vibaya ofisi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Februari 19, 2021 mkuu wa taasisi hiyo Mkoa wa Kagera, John Joseph amesema kesi hiyo namba CC 12/2021 inawakabili watumishi wanne; Dennis Sebugwao meneja mkuu wa Stamigold, Bwire Eliaseph aliyekuwa ofisa manunuzi, Sadick Kasuhya mkuu wa kitengo cha manunuzi na Clara Mwaika mkuu wa idara ya fedha.
Amesema kwa pamoja wakiwa waajiriwa wa kampuni hiyo kati ya Juni 30, 2016 hadi Desemba 31, 2017 walitumia vibaya nafasi zao na kuingia mkataba wa Sh4.6 bilioni na kampuni ya Supercore badala ya mkataba wa Sh3.4 bilioni na kusababisha kampuni hiyo kupoteza zaidi ya Sh1.1 bilioni.
Alieleza kuwa watumishi watatu walipata dhamana lakini Kasuhya alishindwa kutimiza masharti na hivyo kupelekwa rumande.