Umoja wa Mataifa (UN) ulitangaza kuwa kiongozi wa shirika la kigaidi la Al-Qaeda nchini Yemen, Khalid Batarfi, alikamatwa akiwa hai miezi kadhaa iliyopita.
Ndani ya wigo wa UN, "wataalam wanaohusika na ufuatiliaji wa makundi yenye msimamo mkali" walichapisha ripoti juu ya suala hilo.
Katika ripoti hiyo, iliarifiwa kwamba Batarfi, anayejulikana kama "Abu Mikdad al-Kindi", alikamatwa akiwa hai kwenye operesheni iliyoendeshwa El-Gayda, katikati mwa mkoa wa Al-Mehra, mnamo Oktoba mwaka jana, ambapo naibu wake Saad bin Atıf al-Awlaki aliuawa wakati wa operesheni hiyo.
Wakati hakuna taarifa yoyote iliyotolewa katika ripoti hiyo kuhusu maelezo ya wahusika wa walioendesha operesheni hiyo, vyanzo vya Yemen vinasisitiza kuna uwezekano operesheni hiyo iliendeshwa na vikosi vya Saudi Arabia vilivyohudumu Mehra kwa miaka mingi.
Khalid Batarfi alichukuwa nafasi kama kiongozi wa shirika hilo baada ya Qassem er-Rimi, ambaye alikuwa kiongozi wa Al-Qaeda katika Rasi ya Arabia kuuawa mnamo Januari 2020 kwenye shambulizi la chombo cha anga kinachojiendesha cha Marekani.
Batarfi alitoroka na watu wapatao 300 baada ya uvamizi wa gereza katika mkoa wa Hadramawt nchini Yemen mnamo Aprili 2015.