Maalim Seif Akiri Kuugua Corona




Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amefunguka na kueleza kuwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja akisumbuliwa na ugonjwa wa Covid-19.


Alitoa kauli hiyo baada ya mapema jana kuanzia asubuhi kusambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu taarifa za kuwa alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja akisumbuliwa na ugonjwa wa Covid-19.



Chama chake pia cha ACT-Wazalendo nacho kilitoa taarifa baadae ya kuthibitisha kuwa Maalim Seif alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa Covid-19.



Baada ya kusambaa kwa taarifa hizo, Mwananchi iliwatafuta viongozi tofauti wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano kuzungumzia suala hilo.



Msemaji wa Serikali ya Zanzibar, Dk Khalid Salum ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar alisema hawezi kuzungumzia lolote kwa sasa akitaka waulizwe zaidi waliotoa taarifa na kwamba wakati ukifika Serikali itazungumza.



Mapema alitafutwa pia Kaimu Waziri wa Afya wa Zanzibar, Simai Mohamed Said, ambaye pia ni Waziri wa Elimu huko lakini alidai hakuwa na taarifa.



Pia gazeti hili liliwatafuta Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Profesa Dorothy Gwajima, Naibu wake Goodluck Mollel na msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas, ambao wote hawakupatikana.



Hata hivyo, Maalim Seif, ambaye pia ni mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, alithibitishia Mwananchi jana kuhusu kuugua ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona akisema, “Ni kweli niko Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar ambako natibiwa Covid 19. Mke wangu amekuwa `isolated’ (ametengwa) nyumbani,” alisema Maalim Seif kupitia ujumbe mfupi alioutuma kwa mwandishi wa gazeti hili jana usiku.



Kabla ya Maalim Seif kueleza hayo jana mchana chama chake cha ACT-Wazalendo kupitia kwa Katibu Mkuu, Ado Shaibu, aliutangazia umma kuhusu kuugua kwa kiongozi wao, mke wake na wasaidizi wake, ingawa aliongeza anaendelea vyema baada ya kupatiwa matibabu.



“ACT Wazalendo kinawajulisha wanachama wake, Wanzanzibari, pamoja na umma wa Watanzania, kuwa, Maalim Seif Sharif mkewe, Bi Awena, pamoja na wasaidizi wake kadhaa wa karibu, wamethibitika kupata maambukizo ya virusi vya Covid-19 baada ya kufanyiwa vipimo.



“Katika hali ya kuchukua tahadhari zaidi madaktari walimshauri Maalim Seif kuwa ni vyema awepo chini ya uangalizi maalum katika kipindi chote atakachokuwa anaendelea na matibabu dhidi ya corona. Tangu Ijumaa jioni, Maalim Seif alipumzishwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja, Zanzibar, akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari,” alisema Shaibu katika taarifa yake.



Shaibu alisisitiza hali ya Maalim Seif na mkewe zinaendelea vyema huku akiwataka wanachama ACT- Wazalendo Wanzanzibari na Watanzania kumuombea katika kipindi hiki alichopumzishwa ili aweze kupona kwa haraka na arudi kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad