Madeni ya Serikali yanavyotishia mafao ya wastaafu






Sakata la Serikali kudaiwa na mifuko ya hifadhi za jamii jana liliibuka bungeni huku mbunge wa viti maalumu (Chadema), Agnes Kaiza akibainisha kuwa deni hilo ndio sababu ya wastaafu kutolipwa mafao yao kwa wakati.


Hoja ya mbunge huyo ambaye wakati akichangia hotuba ya Rais John Magufuli ya kuzindua Bunge la 12 ilisahihishwa na Mbunge wa Vunjo (CCM), Dk Charles Kimei baada ya kuomba utaratibu, ilitolewa ufafanuzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama aliyekiri Serikali kudaiwa na kuwa inaendelea kulipa.



Kaiza alisema Serikali kudaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kunalitia doa Taifa ambalo kwa sasa limeingia katika uchumi wa kati.



Huku akikiri kazi nzuri inayofanywa na wizara inayosimamia mifuko hiyo, mbunge huyo alikosoa kuwa kumekuwa na ukimya mkubwa unaotia shaka kuhusu malipo hayo, ambayo ni michango ya wafanyakazi.



Sakata la madai ya fedha za mifuko hiyo kwamba zimetumiwa na Serikali, lilianza katika Serikali ya awamu ya nne katika Bunge la 10 pale wapinzani walipolivalia njuga kuwa fedha zimechukuliwa na kupelekwa kwenye miradi isiyokuwa na tija.



Jana katika mchango wake mbunge huyo, alisema mifuko imefilisika hadi inashindwa kulipa fedha za wastaafu ambao waliitumikia nchi kwa muda mrefu wakati kulipwa ni haki yao, lakini hawalipwi.



Alisema kutolipwa kwao kumepelekea wastaafu wawe katika maisha magumu ambayo yanawafanya hata wanajuta kuhusu kile wanachokipata na akataka Serikali ifanye haraka kumaliza matatizo hayo.



Alizungumzia pia kutolipwa kwa madeni ya muda mrefu kwa makandarasi ambao nao wanafanya shughuli za maendeleo ndani ya Taifa kwamba yanatokana na kutokuwepo kwa fedha.



“Si wastaafu pekee, hata makandarasi tunaona kila kukicha wabunge wanalia kuhusu makandarasi wanaoendelea na kazi majimboni mwao, kwamba hawalipwi na yote inatokana na madeni ya ndani ikiwemo mifuko,” alihoji Kaiza.



Katika majibu yake, Mhagama alisimama akitumia kanuni ya 70 kumpa taarifa mbunge huyo huku akikiri kuwa Serikali bado inadaiwa lakini inaendelea kuyashughulikia madeni hayo hatua kwa hatua.



Mhagama alisema hadi sasa Serikali imeshalipa Sh1.2 trilioni kwa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na inaendelea kuhakiki madeni mengine kabla ya kuanza kuyalipa.



Waziri alisema Serikali ya awamu ya tano haikurupuki kulipa madeni bila ya kufanya uhakiki, hivyo ikikamilisha mchakato wa kuyahakiki italipa wakati wowote.



Hata hivyo, hakutaja ni kiasi gani Serikali inadaiwa na mifuko hiyo lakini alisisitiza kuwa hata wastaafu wameanza kulipa na akaahidi kwamba ataandaa taarifa sahihi kuwajulisha wabunge kuhusu malipo na kiasi ambacho Serikali bado inadaiwa.



“Napenda mbunge afahamu kama ambavyo nilieleza kwenye kamati nilipokwenda na wataalamu, kwamba tumeshalipa kwa PSSSF Sh1.2 trilioni na fedha hizo zimerudishwa kwao, lakini madeni mengine tunaendelea kuyashughulikia kwa kufanya uhakiki kwanza,” alisisitiza.



Kaiza alikiri kupata taarifa za malipo hayo lakini akasisitiza kwamba bado kuna madeni makubwa ambayo Serikali inadaiwa na ndiyo yanayoangukia kwenye kundi la uhakiki alilosema Waziri, hivyo akahoji lini uhakiki huo utakwisha.



Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2017/18 iliyotolewa Machi 2019, ilisema Serikali ina deni ya jumla ya Sh 2,390.08 bilioni (zaidi ya trilioni 2 kwenye mifuko sita ya hifadhi ya Jamii, ambapo kiasi cha Sh1,625.25 bilioni (sawa na asilimia 68) kilipaswa kiwe kimelipwa katika mwaka wa fedha 2017/2018.



“Mikopo mingine iliiva tangu mwaka 2014. Kuchelewa kulipwa kwa mikopo hiyo kumeathiri uendeshwaji wa mifuko husika,” ilieleza ripoti hiyo.



CAG alisema mfuko mpya wa watumishi



wa umma (PSSSF)) umebeba madeni ya mifuko iliyoungana, ambayo yanaweza kuhatarisha ukwasi wake.



Katika taarifa yake, Dk Kimei alisema anachokizungumza mbunge huyo kwa kuhusisha madai na kuingia kwa Tanzania katika uchumi wa kati hakina uhalisia.



“Huwezi kufananisha mambo hayo, hivyo ni vitu viwili tofauti kabisa, hata nchi zilizoingia katika uchumi wa juu bado zina madeni ya kudai na kudaiwa, hivyo haitakuwa ajabu kwa Tanzania.



Hata hivyo, Kaiza alikataa taarifa hiyo akisema haina ukweli kwa kuwa suala la kuingia katika uchumi wa kati linamaanisha kuna maendeleo yaliyopigwa ndani ya Taifa. na tafsiri yake ni kuwa pato limeongezeka kwa kiasi, hivyo kubaki na madeni ya watu waliolitumikia Taifa inatia doa na kuonyesha kwamba kuna mahali watu hawajali.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad