Madiwani Uyui waagiza kusakwa Mtendaji aliyetoweka na milioni 10






Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Uyui Mkoani Tabora wamemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Hemed Magalu kumsaka Mtendaji wa kijiji cha Nh’umbo, kata ya Igulungu, Isack Malio aliyetoweka na fedha za mapato Sh milioni 10.


Wametoa agizo hilo jana katika kikao cha kwanza cha robo ya pili ya Baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.



Diwani wa kata hiyo, Kulwa Lushika, alisema kuwa fedha hizo zilichangwa na wananchi mwaka jana kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika shule ya msingi Nh’umbo ambapo baada ya kukusanya fedha hizo alitoweka nazo.



Aliongeza kuwa baada ya kuulizwa na wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji hicho (VDC) kuhusu michango hiyo aliwaeleza kuwa ziko benki na alipotakiwa kwenda kuleta karatasi ya benki (Bank Slip) alitokomea moja kwa moja.



Alibainishwa kuwa kila kaya ilichangia kiasi cha Sh 30,000 kwa ajili ya mradi huo ambapo zilipatikana jumla ya sh mil 10 lakini Mtendaji huyo akakaa nazo badala ya kuzipeleka benki ili kutekeleza shughuli iliyokusudiwa.



“Kitendo hicho kimetuumiza sana na kimerudisha nyuma shauku ya wananchi kuchangia shughuli za maendeleo, tumeshatoa taarifa wilayani kwa ajili ya hatua zaidi ikiwemo kusakwa kokote aliko ili kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema.



Diwani wa kata ya Nsololo, Habib Sungwa na mwenzake wa kata ya Isikizya, Ally Mtelela walisema kuwa kitendo kilichofanywa na Mtumishi huyo hakifai na hakikubaliki hivyo wakamtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya dola kumsaka kokote aliko ili sheria ichukue mkondo wake.



Awali, diwani wa viti maalumu kata ya Igulungu, Elizabeth Makongoro, aliomba ufafanuzi kutoka kwa DED wa halmashauri juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya mtumishi huyo ambapo DED alieleza kuwa suala hilo wameshalipata na wamelifikisha TAKUKURU na jitihada za kusakwa mtendaji huyo zinaendelea.



Akihitimisha hoja hiyo Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Shaban Katalambula ambaye ni diwani wa kata ya Goweko aliagiza Ofisi ya Mkurugenzi kumsaka kokote aliko na fedha hizo zirejeshwe.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad