Nchi wanachama wa Mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za Uhalifu ya ICC zinajiandaa leo ijumaa kumchagua mwendesha mashtaka mkuu wa taasisi hiyo ya kimataifa.
Kuna wagombea wanne wanaowania nafasi hiyo kutoka Uingereza,Jamhuri ya Ireland, Italia na Uhispania.
Fatou Bensouda anayeshikilia nafasi hiyo kwa sasa amewekewa vikwazo na Marekani.Mgombea kutoka Uingereza Karim Khan anatajwa kuwa na uwezekano mkubwa wa kuchaguliwa katika nafasi hiyo ya muhula wa miaka tisa akimtangulia mgombea wa Uhispania Carlos Castresana.
Nchi wanachama wa ICC zilishindwa kufikia maelewano kuhusu nafasi hiyo licha ya kujaribu wiki za hivi karibuni na sasa watapiga kura huko New-York katika Umoja wa Mataifa.
Muda wa Mwendesha mashataka mkuu Fatou Bensouda raia wa Gambia utamalizika mwezi Juni na atakayeingia atarithi mrundo wa kesi ngumu ikiwemo uhalifu wa kivita Afghanistan, na uchunguzi kuhusu vita kati ya Israel na Gaza vya 2014.