Maskini Liverpool Pumzi imekata …



Liverpool, England. MAISHA yanakwenda kasi kwelikweli. Liverpool ile iliyokuwa moto wa kuotea mbali na kupewa nafasi kubwa ya kutawala soka la England kwa muda mrefu, msimu mmoja tu wa kutoka kubeba ubingwa kwa kishindo, hali si shwari.

Baada ya kiwango matata kabisa cha misimu miwili iliyoshuhudia Liverpool ikivuna karibu pointi 200 kwenye Ligi Kuu England, ikiwamo msimu uliopita walipomaliza ukame wa miaka 30 ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England, mambo yamekuwa tofauti sana katika msimu huu wa 2020-21.


Kulikuwa na maneno kwamba Liverpool ingekuwa bora zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu England, lakini kwa sasa wanapambana walau wamalize ndani ya Top Four ili kulinda hadhi yao.

Kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Brighton Jumatano iliyopita hakikuwa bahati mbaya, bali kilikuwa kipigo cha pili mfululizo Liverpool ikipokea kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Anfield, baada ya mechi 68 za ligi bila ya kupoteza uwanjani hapo.

Majeruhi yanatajwa kuwa sababu, hasa kwenye safu yao ya mabeki ambapo itawakosa kwa muda mrefu mabeki wa kati, Virgil van Dijk, Joe Gomez na Joel Matip. Hata fowadi yao pia imekuwa butu.

Ukilinganisha mechi 22 za msimu uliopita kwenye ligi na za msimu huu wakiwa wamefikisha idadi hiyo ya mechi, mambo ni tofauti kabisa.

Rekodi yao ya ushindi kwenye mechi hizo 22, msimu huu Liverpool imeshinda 11 tu, huku ikifunga mabao tisa pungufu na kuruhusu wavu wao kuguswa mara 11 zaidi.


Hata hivyo, kwenye beki ya miamba hiyo inayonolewa na Jurgen Klopp kwa msimu huu imekabiliana na mashuti machache ukilinganisha na msimu uliopita, ambapo mashuti yameshuka kutoka 280 hadi 180.

Lakini, ubora huo wa mashuti waliyokabiliana nayo ubora wake umekuwa tofauti, msimu uliopita kwenye mechi 22 walikuwa wamekabiliwa na mashuti 59 yaliyolenga goli, lakini kwa msimu huu mashuri yaliyolenga goli lao ni 76.


Tatizo lipo kwenye fowadi pia, ambapo kuna kiwango kibovu kwenye usahihi wa mashuti yao wanayopiga. Kwenye mechi 22 za mwanzo za msimu uliopita wa 2019-20 na huu wa 2020-21, takwimu zake zinasomeka hivi.

Kwa msimu uliopita, kwenye mechi hizo 22, Liverpool ilikuwa imeshinda 21 na kutoka sare moja tu, lakini msimu huu kwenye mechi hizo, imeshinda 11, sare saba na vichapo vinne.

Kwa msimu uliopita kwenye mechi 22, Liverpool ilikuwa imefunga mabao 52, imefungwa 14 na kuwa na wastani wa tofauti ya mabao wa chanya 38, lakini msimu huu imefunga mabao 43, imefungwa 25 na kuwa na wastani wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa chanya 18. Kwenye mechi hizo, msimu uliopita Liverpool ilivuna pointi 64, ilipiga mashuti 347 na yaliyolenga goli ni 136, lakini kwa msimu huu, imevuna pointi 40, imepiga mashuti 345 huku yaliyolenga goli ni mashuti 124.

Kwa msimu huu imekumbana na mashuti machache 180 ukilinganisha na msimu uliopita mashuti 208, lakini tofauti ni kwamba msimu huu mengi yamelenga golini, 76, wakati kwa msimu uliopita, mashuti yaliyolenga kwenye goli lao katika mechi hizo 22 yalikuwa 59. Eneo ambalo Liverpool imefanya vizuri kwa msimu huu hadi sasa ni kwenye kupiga pasi, ambapo katika mechi hizo 22, imepiga pasi 14,643 na zilizofanikiwa kufikia walengwa ni 12,615 wakati kwa msimu uliopita kwenye idadi kama hiyo ya mechi, ilipiga pasi 13,380 na sahihi zilikuwa pasi 11,208.

Liverpool kesho Jumapili itakuwa uwanjani kwao Anfield kuwakabili vinara wa ligi, Manchester City. Jurgen Klopp na chama lake hilo la Liverpool atahitaji ushindi ili kupunguza pengo la pointi, ambapo kwa sasa wakishika namba nne apo nyuma kwa pointi saba, huku wakiwa wamewazidi Chelsea waliopo kwenye nafasi ya sita kwa pointi nne tu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad