Mbunge wa viti maalum wa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Nusrat Hanje amemuomba Rais Dkt. John Magufuli kuzifuta kesi zote zinazohusu uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2020 ili wananchi wafanye shughuli za kuijenga nchi.
Hanje ni miongoni mwa wanawake 19 waliovuliwa uanachama wa Chadema baada ya kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum bila ridhaa ya chama hicho. Baada ya kufukuzwa uanachama walikata rufaa na sasa kikao cha Baraza kuu la Chadema kinasubiriwa kusikiliza rufaa yao na kutoa uamuzi.
Licha ya Chadema kutowatambua, lakini waliapishwa na Spika Job Ndugai na sasa wanashiriki vikao vya Bunge la 12 vinavyoendelea mjini Dodoma.
Akizungumza bungeni jana Jumatano Februari 3, 2021 katika mjadala wa hotuba ya ufunguzi wa Bunge ya Rais Magufuli aliyoitoa mwishoni mwa 2020, Hanje amesema wanasiasa kuendelea kwenda mahakamani wakati uchaguzi umekwisha hakutoi taswira nzuri kwa mataifa mengine.
Amewataja baadhi ya wanasiasa wenye kesi mahakamani kuwa ni naibu katibu mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui na kada wa Chadema, Salome Makamba.
“Yaani mtu umemchukulia mke wake halafu bado unataka kumuua hilo jambo siyo sawa kabisa, ufike wakati wahusika watambue hilo ili watu wakae kupanga namna ya kulijenga taifa lao,” amesema Hanje.
Amesema anao uzoefu wa vitendo kwa maisha ya gerezani kutokana na muda aliokaa mahabusu kwa sababu za kisiasa. Amebainisha kuwa maisha ya gerezani hayafai hasa katika kipindi hiki ambacho kuna tishio la ugonjwa wa Uviko 19. Kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 amesema kila mmoja anajua ndani ya moyo wake kilichotokea.
Hanje aliapishwa kuwa mbunge siku moja baada ya kutoka mahabusu alikoishi kwa siku 133. Yeye na wenzake walishtakiwa kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usio halali, kudhihaki wimbo wa Taifa, kujaribu kuvujisha siri za halmashauri ya wilaya ya Ikungi mkoani Singida na kutoa lugha za kuudhi.
Novemba 23, 2020 walitoka gerezani baada ya kufutiwa mashtaka na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga.