Mbunge wa Mbulu Mjini (CCM), Zacharia Isaay ametaka Serikali ya Tanzania kueleza wazi kuhusu alichokiita ugonjwa wa kupumua ambao anasema unamaliza watu wa Mbulu.
Isaay amezungumza kwa hisia kali bungeni leo Alhamisi Februari 11,2021 akisema hawezi kuzungumzia mpango badala yake anaona bora azungumzie hali ya wananchi wake ambao kila mara anakwenda kuzika.
“Serikali iache kigugumizi jimboni kwangu watu wanakwisha Spika,nimechoka kuzika hata leo wanazika mtoto wa diwani wakati mwingine nashindwa kukuaga Spika kwenda Mbulu naamua kutoroka,” amesema Isaay.
Mbunge huyo anasema wanaopoteza maisha jimboni kwake magonjwa yao yanafanana ambayo ni tatizo la kupumua akihofia kuwa msimu wa baridi jimboni kwake utaendelea kuwaumiza.
“Jana nilikwenda hospitali ya hapa Benjamin Mkapa (Dodoma) kwa ajili ya kufanya vipimo lakini wakaniambia mitungi ya gesi imejaa,watu ni wengi sasa nimesema kama watu watanichukia basi lakini nimesema,” amesema Isaay.
Mbunge huyo ameomba Serikali kuangalia namna ya kuboresha dawa za miti shamba ambazo ameeleza kuwa zinasaidia kwa kiasi kikubwa lakini akabainisha kuwa zinapatikana kwa gharama kubwa.