SIKU Tatu baada ya Rais Dk John Magufuli kuwataka watanzania kuchukua tahadhari huku wakimtanguliza Mungu kwa sala, dua na maombi juu ya ugonjwa wa kushindwa kupumua, Mbunge wa Singida Magharibi ametoa maoni yake kuhusu kauli hiyo akimpongeza Rais Magufuli kwa kuwa Kiongozi mwenye imani thabiti ya kiroho.
Akizungumza na Michuzi Blog, Kingu amesema kauli ya Rais Magufuli aliyoitoa wakati wa ibada ya kumuaga Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi John Kijazi inaonesha jinsi gani ambavyo amekua ni mnyenyekevu mbele za Mungu na mwenye kumtanguliza mbele katika kila kitu jambo ambalo viongozi wengi hawana.
Kingu amesema kauli hiyo ya Rais Dk Magufuli imeleta tumaini jipya kwa watanzania ambao walikua wametawaliwa na hofu huku wakitishwa na kujazwa hofu na baadhi ya watu ambao wamekua hawana mapenzi mema na Tanzania.
" Tunaweza tukakejeli tunaweza tukadharau tunaweza kusema kwa namna yoyote lakini ukweli ni kwamba mwisho wa yote Mungu ni mkuu wa kila jambo na mamlaka zake ni kuu, Rais amesema tuombe tumrudie Mungu kila mmoja kwa imani yake hilo ni jambo la kipekee na ninaamini linaweza kulirudisha Taifa katika hali nzuri.
Rais Dk Magufuli ameonesha jinsi gani amekua akimtumaini Mungu kwenye kila jambo na ndio maana amekua na uthubutu hata wa kupambana kulinda rasilimali za Taifa letu, kupambana na rushwa, ufisadi na kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati kama mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR pamoja na kuhamishia Serikali Makao Makuu ya Nchi Dodoma, uthubutu wote huu umeletwa na imani yake thabiti kwa Mwenyezi Mungu," Amesema Kingu.
Amesema kiburi cha mali, Sayansi kimewafanya watu wasahau uwepo wa Mungu lakini uwepo wa Mungu ni kipekee hivyo kuwataka watanzania wote kuiunga mkoni kauli hiyo ya Rais na kumrudia Mungu kwani hata Mwaka jana kupitia maombi ugonjwa huo uliondoka nchini.
" Unadhani kwanini mwanzo tuliweza kuhimili hali hii kiasi cha kushangaza mataifa makubwa ambayo yalishindwa? Tuliweza kwa sababu tulijikabidhi kwa Mungu hivyo mimi namuunga mkono Rais wetu kwamba tufanye ibada tumlilie Mungu wetu," Amesema Kingu.