Dar es Salaam. Sare ya tatu mfululizo kwa Yanga juzi imekuwa mwiba mchungu kwa kocha Cedric Kaze, huku mashabiki wakiwa na hasira juu ya upangaji wake.
Kaze, ambaye ameiongoza Yanga kucheza bila kupoteza mchezo wowote wa kimashindano, alijikuta katika wakati mgumu baada ya kikosi chake kutangulizwa kwa mabao 3-2 baada ya dakika 45 na Kagera Sugar.
Mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3 ulimfanya Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla kutoka chini ya ulinzi baada ya mashabiki waliokuwa na hasira kumzonga.
Lakini lawama pia zilikwenda kwa Kaze, ambaye kwa mshangao aliamua kumwacha nje kiungo mkabaji, Mukoko Tonombe na kumtumia Zawadi Mauya katika kiungo.
Uamuzi huo ulionekana mapema ndani ya dakika 20 za kwanza kutokana na kikosi chake kuwa na kazi ya kusawazisha kila bao lililokuwa likifungwa na Kagera Sugar walioonekana kuvuruga eneo la katikati.
Nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella alielekeza lawama zake moja kwa moja kwa kocha Kaze, kwamba majaribio yake yamemgharimu kwa kumuacha Mukoko nje, ambaye alibadilisha mchezo baada ya kuingia.
“Nimeona kauzembe fulani kwa kocha, huwezi kumuacha mchezaji kama Mukoko nje wakati unatafuta matokeo ya kujilinda kileleni, hii inaonyesha ni namna gani wachezaji wetu wazawa wasivyojitambua na kuwapa heshima wageni, ushauri wangu, Kaze awe na kikosi cha ushindani, mashabiki wanaumia na matokeo, tayari anaipa Simba nafasi ya kukaa kileleni,” alisema.
Kauli yake iliungwa mkono na aliyekuwa beki wa timu hiyo, Bakari Malima kwamba hakukuwa na haja ya Kaze kumuacha benchi Mukoko, ambaye baada ya kuingia alionekana kuwasumbua Kagera Sugar.
“Msaidizi wake, Nizar Khalfan anapaswa kumshauri sana Kaze, kwani amecheza anajua ligi ikiwa mzunguko wa pili inakuwa na ushindani wa kiasi gani, ingawa nawalaumu na wachezaji waliopewa nafasi hawana muendelezo wa kutunza viwango vyao,” alisema.
Kwa upande wake, winga wa zamani wa Yanga, Edbily Lunyamila alimshauri Kaze kuwa na kikosi cha kusaka ushindi hasa kwenye timu ngumu kama Kagera Sugar. “Ingawa siwezi kuzungumza sana, kocha atakuwa amejua ni wapi alipokosea atajipanga kwenye mechi zinazokuja ili makosa yasijirudie, kikubwa ajue mashabiki wanahitaji ubingwa ambao wameukosa ndani ya misimu mitatu,” alisema Lunyamila.