Na Clavery Christian Bukoba Kagera.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Kagera TAKUKURU imefanikiwa kuzima mpango wa Uhujumu uchumi katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF kwa madai hewa yaliyo wasilishwa na maduka mawili ya dawa yakidai kulipwa shilingi milioni 294 kinyume na utaratibu na kufanikiwa kurejesha fedha zote zilizokuwa zimeisha lipwa kwa maduka hayo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa Kagera Bw, John Joseph akiongea na waandishi wa habari mbele ya mkuu wa mkoa Kagera Brig. Jen. Marco E Gaguti amesema kuwa fedha hizi zimeweza kuokolewa kutokana na ufatiliaji uliofanyika kutokana na kupokelewa kwa taarifa kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF ambapo katika ufatiliaji TAKUKURU ilibaini kuwa fedha hizo zimetokana na madeni hewa yaliyokuwa yamewasilishwa na maduka mawili ya madawa yakionyesha kuwa kati ya mwezi Mei na Novemba mwaka 2016 yalitoa madawa kwa wagonjwa yenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni 304, 601, 376.
"Ufatiliaji wetu ulibaini kuwa madai hayo yalikuwa ya uongo kwa kuwa fomu za Bima ya Afya zilizowasilishwa zilikuwa zimeandikwa na mtu anayedaiwa kuitwa Dr. Frida Samweli ambaye siyo Daktari na wala siyo mtumishi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa Kagera na hatambuliki, kwa maana hiyo ziliandaliwa kwa nia mbaya ya kutaka kufanya udanganyifu, Kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007" alisema John Joseph mkuu wa TAKUKURU Kagera.
Bw, John Jeseph ameyataja maduka hayo ya dawa kuwa ni MK PHARMACY duka la dawa linalomilikiwa na Murtaza Pathan liliokuwa limewasilisha hati ya mafai ya shilingi milioni 231, 994, 548 na kulipwa shilingi milioni 10, 198, 685 na kuendelea kudai milioni 221, 795, 863. Duka jingine ni EJU ENTERPRISES linalomilikwa na Erick Mugisha Kiiza lililokuwa limewasilisha hati ya madai yenye thamni ya shilingi milioni 72, 606, 828 na kulipwa kiasi cha shilingi 169, 800 na kuendelea kudai shilingi milioni 72, 437, 028.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brig. Jen. Marco E Gaguti akikabidhi fedha hizo zilizookolewa na TAKUKURU Mkoa Kagera jumla ya shilingi milioni 10, 368, 400 katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ameiopongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa Kagera kwa kazi kubwa wanayifanya ambapo wameweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha na kuwasaidia watu wengine. RC Gaguti ameitaka TAKUKURU mkoa Kagera kuhakikisha wanafanya uchunguzi mpaka wote waliohusika wanakamatwa na kugikishwa katika vyombo vya sheria na kuwataka watumishi wa umma kujiepusha na vitendo vya Rushwa kwani zama hizi siyo zama walizozoea za kipindi kile.