Jeshi la Angani la Marekani litapitia tena mifumo ya usalama duniani baada ya mvamizi kuingia eneo la chini kunakohifadhiwa ndege inayombeba rais, maarufu Air Force One.
Alhamisi, mwanamume ambaye hakuwa na silaha alifanikiwa kuingia kisiri katika kambi ya jeshi ya Andrews iliyopo Maryland na kupanda ndege aina ya C-40, ambayo hutumika na viongozi wa serikali.
"Kila mmoja analichukulia hili kwa umuhimu mkubwa," amesema msemaji wa wizara ya ulinzi John Kirby siku ya Ijumaa.
Hakuna chochote kinachoonesha kwamba mvamizi huyo ana uhusiano na makundi ya kigaidi.
Mvamizi huyo alikamatwa na anazuiliwa na vikosi vya usalama katika kambi hiyo, kulingana na taarifa kutoka kikosi cha jeshi la angani.
Alitakiwa kufika mahakamani kwa makosa ya kuingia eneo hilo bila ruhusa na kukabidhiwa watekelezaji sheria wa eneo.
Hakuna aliyedhurika wakati wa ukiukaji huo wa sheria.
Inasemekana kuwa siku za nyuma, tayari kulikuwa kumetolewa vibali viwili vya kukamatwa kwa mvamizi huyo ambavyo havikuwa vimetekelezwa lakini hakuna taarifa zaidi zilizotolewa.
Kambi ya jeshi ya Andrews ipo kilomita (24) kutoka Ikulu ya Marekani, Washington, DC, na mara nyingi huwa inatumika na rais, makamu rais na viongozi wengine wa Marekani.
Rais Joe Biden alisafiri kupitia kambi hiyo hadi nyumbani kwake Wilmington, Delaware, Ijumaa usiku.