Jeshi la Myanmar limetangaza hali ya dharura likidai udanganyifu wa kura katika uchaguzi, baada ya kuwakamata viongozi kadhaa akiwemo Aung San Suu Kyi.
Jeshi la Myanmar limetangaza hali ya dharura kwa muda wa mwaka mmoja na kumuweka jenerali wa zamani kama rais, kimetangaza Jumatatu kituo cha televisheni cha Myawaddy kinachomilikiwa na jeshi.
Jenerali wa zamani Myint Swe, ambaye awali alikuwa makamu wa rais, ametangazwa kama kaimu rais.
Hata hivyo, katika hali hiyo ya dharura kamanda mkuu wa jeshi Min Aung Hlaing amechukuwa udhibiti kamili wa nchi hiyo.
Tangazo hilo la jeshi limetolewa kufuatia kukamatwa kwa kiongozi wa Myanamar Aung San Suu Kyi baada ya siku kadhaa za mivutano nchini humo iliyozua hofu ya kutokea mapinduzi.
Rais Win Myint na viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa chawa tawala pia wamekamatwa mapema Jumatatu, amesema Myo Nyun msemaji wa chama hicho cha National League for Democracy .
Akizungumza kwa njia ya simu na shirika la habari la dpa, Nyun amesema wakati wowote naye anaweza kukamatwa na wanajeshi hao.
Tangu wiki iliyopita jeshi la Myanmar limekuwa likitishia kufanya mapinduzi kwa madai kwamba kulifanyika udanganyifu katika uchaguzi uliopita wa mwezi Novemba uliokipa ushindi chama cha Suu Kyi cha NLD.