KIKOSI cha Namungo FC kimerejea hotelini usiku wa kuamkia leo Februari 14 baada ya kushindwa kuondoka jijini Luanda, Angola kurejea Tanzania ikitumia kutwa nzima ya jana ikiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Luanda.
Namungo imeshindwa kusafiri kwa ndege ya kukodi baada ya wachezaji wake watatu na kiongozi mmoja ambao inadaiwa waliokutwa na maambukizi ya virusi vya #Corona kutoruhusiwa na mamlaka kutoka karantini kujiunga na wenzao kwa ajili ya safari hiyo.
Awali Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliufuta mchezo huo wa Kombe la Shirikisho kati ya CD de Agosto ya Angola dhidi ya Namungo FC ya Tanzania uliopangwa kufanyika jana Februari 14.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), sababu za kufutwa mchezo huo ni taratibu za #COVID19 ambapo mamlaka za Angola ziliutaka msafara wa timu yote ya Namungo kuwekwa karantini mara baada ya kuwasili nchini humo.