Ndege ya Marekani yadondosha mabaki ya injini eneo la makazi Denver




 Ndege ya Boeing ililazimika kudondosha mabaki ya injini yake katika eneo la makazi mjini Denver, Marekani baada ya injini yake kukumbwa na hitilafu ya kiufundi wakati wa kupaa.


Ndege hiyo ya Boeing 777, iliyokuwa na abiria 231 na wafanyakazi 10, ilifanikiwa kutua salama katika uwanja wa ndege wa Denver. Hakuna majeruhi waliyoripotiwa.




Polisi katika mji wa Broomfield waliweka mtandaoni picha zinazoonekana kuwa mabati ya sehemu ya mbele inayofunika injini katika bustani ya nyumba moja.



Wasafiri waliyoabiri ndege hiyo walielezea kuwa "walisikia mlipuko mkubwa" mara baada y andege kupaa angani.





Ndege hiyo yenye nambari ya usajili 328, inayomilikiwa na shirika la ndege la United ilikuwa safarini kuelekea Honolulu, injini yake ya upande wa kulia ilipokumbwa na hitilafu, Mamlaka ya usafiri wa angani ya nchini Marekani (FAA) imesema.



Mmoja wa abiria aliyekuwa ndani ya ndege hiyo ameiambia shirika la habari la AP kwamba rubani alikuwa akitoa tangazo wakati mlipuko mkubwa ulisikika.



"Ndege ilianza kuyumba yumba vikali, mara ikaanza kushuka chini," David Delucia alisema.



Aliongeza kuwa yeye na mke wake waliweka stakabadhi za utambulisha mfukoni "ili ndege ikianguka, tuweze kutambuliwa"



Picha zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha moshi ukifuka kutoka kwenye injini ya ndege hiyo. Moja ya video inayodaiwa kunaswa kutoka ndani ya ndege hiyo inaonesha injini ikiwaka moto na sehemu iliyofunika sehemu.



Kisa hicho kilitokea saa (20:00 GMT) siku ya Jumamosi.



Polisi wa Broomfield wametoa wito kwa wakaazi wa eneo hilo kutogusa au kuondoa mabaki hayo. FAA na Bodi ya Kitaifa ya Usalama wa Uchukuzi itafanya uchunguzi.



Mkaazi wa Broomfield aliiambia CNN kwamba waliona vitu vikianguka kutoka kwa ndege hiyo wakaamua kuingia nyumbani yeye na watoto wake kwa kuhofia wasidhurike.



"Tuliona kitu kikidondoka kutoka angani, kisha tukasikia mlipuko mkubwa, tulipoangalia juu tuliona moshi mweusi angani," Kieran Cain alisema.



"Baada ya hapo vitu zaidi vilianza kudondoka, ilionekana kama vitu vilivyokuwa vikielea kuja chini na havikuwa na uzito, lakini sasa tumebaini, ni vipande vya vyuma vikubwa ambavyo vimeenea kila mahali."

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad