Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema mikopo inayotolewa na Serikali kwa wanafunzi wa elimu ya juu imegeuka biashara.
Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo Alhamisi Februari 11, 2021 na kubainisha kuwa riba inayodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) inakuwa mzigo na wanaoumia zaidi ni watoto wa masikini.
Miongoni mwa malalamiko yanayotolewa na wadaiwa ni ongezeko la makato ya mkopo huo kutoka asilimia 8 hadi asilimia 15 kwa mwezi kutoka katika mshahara ghafi wa mdaiwa/mnufaika.
Mengine ni tozo ya kutunza thamani ya mkopo ya asilimia 6 (Value retention fee -VRF), tozo ya asilimia moja ya shughuli za kiutalawa (Loan Administration Fee) na adhabu ya asilimia 10 ya deni linalodaiwa kwa anayechelewa kulipa deni baada ya miaka 2 tangu kuhitimu chuo.
"Hii ni kweli maana kumpa mtoto wa masikini mkopo wa elimu halafu unakuja kumdai mkopo na riba sio sawa hiyo ni sawa na biashara," amesema Ndugai.
Spika amesema utaratibu huo hauendani na kauli ya kuwasaidia wanafunzi na kwamba utaratibu huo hauna tofauti na wanaokopa fedha za kununua magari.
Ndugai alieleza hayo wakati akiunga mkono hoja ya mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Ramadhan Ihondo aliyependekeza riba kuondolewa katika mikopo ya elimu ya juu.
Ihondo amesema Serikali haiwasaidii vijana wa Kitanzania katika elimu bali inawakomoa kutokana na riba kubwa wanayochukua katika mikopo yao.