Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila ametoa ripoti ya uchunguzi wa kifo cha dereva wa lori Abrahaman Issa (61) ikieleza kuwa alifariki kwa ugonjwa wa homa ya mapafu huku huku familia ikikubali shingo upande.
Suala hilo limezua vuta nikuvute kati ya polisi na madereva wa malori kuhusu kifo cha mwenzao, wakisema Issa alikufa mikononi mwa polisi huku polisi wakisema alikufa kwa maradhi hayo.
Mjomba wa Marehemu, Faisal Hassan, alisema kwa sasa wamekubaliana na kauli ya Serikali kwa kuwakabidhi mwili wa marehemu na kufuata taratibu zote walizoelekezwa kumsitiri katika makaburi ya Uyole jijini hapa.
“Kwa sasa tupo kumswalia katika msikitini na baada ya hapa tutakwenda makaburini kumsitiri na tukimaliza tutajua nini kinaendelea kwani si jambo jema kwa dini yetu ya mtu kukaa zaidi ya siku tatu bila kuzikwa,” alisema jana.
Alisema familia ya marehemu kwa sasa hawapo Mbeya ila baada ya mazishi watapeleka msiba nyumbani kwake Dar es Salaam.
“Kimsingi kwa sasa acha tumsitiri mjomba lakini mambo mengine tutajua tunafanyaje lakini kuhusu kauli hiyo ya Serikali bado inatupa mashaka ingawa kifo tumeumbiwa wanadamu.
ADVERTISEMENT
Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Madereva wafanyakazi wa Malori, Abubakar Msangi alisema kwa sasa hawatoweza kuzungumza chochote kwani kitendo kilichotokea Mungu anajua.
Chalamila aliunda kamati ya watu saba iliyoanza kazi Januari 28 kuchunguza ukweli wa mkanganyiko huo.
Akisoma taarifa ya uchunguzi huo mjini Mbeya jana, Chalamila alisema Issa alikuwa akisumbuliwa na pumu na alikufa kutokana na homa ya mapafu.
Alisema Januari 27 jioni Issa akiwa njiani alijisikia vibaya na hivyo mmoja wa ndugu zake waliyekuwa safari moja kutoka Dar es Salaam kwenda DRC alishauri washuke katika Hospitali ya Mission ya Chimala wilayani Mbarali kwa matibabu.
Baada ya kuchukuliwa vipimo daktari aliyekuwa zamu alibaini ana homa ya mapafu na kushauri atengwe na kulazwa, lakini aligoma akisema atakwenda kupatiwa matibabu Tunduma.
“Baada ya kuondoka aliendelea kuendesha gari huku likiyumba na kugonga magari mawili ndipo polisi walimfuatilia na kumkamata kwa nguvu na baadaye alipozidiwa na homa ya mapafu alikufa akipelekwa hospitali.
Baada ya kufikishwa kituo cha polisi, Chalamika alisema hali yake iliendelea kudhoofika ndipo askari waliokuwa zamu walimpeleka Kituo cha Afya Igawilo lakini alifikishwa akiwa tayari amefariki dunia.