Timu ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 20 'Ngorongoro Heroes', saa 4:00 usiku wa leo Februari 22, 2021 inataraji kushuka dimbani kucheza dhidi ya Morocco U20 kwenye mchezo wa mwisho kundi C kuwania nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya AFCON U20 nchini Mauriatania.
Kuelekea kwenye mchezo huo ambao Ngorongoro Heroes wanahitaji ushindi ili kuweka hai matumaini ya kutinga hatua hiyo, Nahodha wa timu hiyo Kelvin John amesema wanaamini watafuzu kutokana na walivyojipanga kwenda kupata matokeo mazuri.
“Tunajua Morocco ni timu nzuri na sisi tumejipanga kwenda kupata matokeo kwenye mchezo huo, bado tuna nafasi kubwa ya kuweza kupata matokeo kwahiyo, kikubwa zaidi tunapokea maelekezo vizuri kutoka kwa mwalimu wetu na mipango yake ili tuweze kufanya vizuri kwenye mchezo huo”.
Kwa upande wa kocha wa kikosi hicho, Jamhuri Kihwelo 'Julio', amesema “Tunakutana na Morocco, hatuogopi ushindani huu uliopo kwa wenzetu waliotangulia kabla yetu, lakini tunasema tu, kubwa tunataka tushinde ili tupate nafasi ya kuendelea”.
Ngorongoro Heroes ikipata ushindi, itafikisha jumla ya alama 4 na kuombea mchezo wa Gambia dhidi ya Ghana utakaochezwa muda mmoja umalizike kwa sare ili wamalize nafasi ya tatu na kufuzu kwakuwa 'Best loser' kwani Tunisia kutoka kundi B imefuzu ikiwa best loser kwa kuwa na alama 4.
Kundi A, wenyeji Mauritania wameshika nafasi ya tatu wakiwa na alama 3 hivyo wataweza kufuzu hatua ya robo fainali endapo Ngorongoro Heroes na Gambia kutoka kundi C watafungwa ama kutoka sare na wawili hao kusalia na alama mbili mbili.
Timu tano zilizofuzu kucheza hatua ya robo fainali ni, vinara wa kundi A, Cameroon, Uganda walioamliza wapili, Kundi B, Burkina Faso, Central Afrika na Tunisia ikiwa ni 'Best loser'.
Hatua ya robo fainali ya michuano hii ambayo Ngorongoro Heroes wanashiriki kwa mara ya kwanza, inatazamiwa kuchezwa siku ya Alhamisi ya tarehe 25 Februari 2021 nchini Mauritania ambao ndiye wenyeji wa michuano hiyo.