WENYE mapenzi yao wanasema umri ni namba tu kwani si kigezo kikubwa cha kuzingatia linapokuja suala la mapenzi ya dhati kutoka moyoni.
Hadi hapa tulipofikia, staa wa Bongo Fleva, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ anakiri kwa kinywa chake mwenyewe kwamba hajiwezi kwa mwanamama mkali wa Bongo Movies, Kajala Masanja ambaye amemzidi umri.
Kwa sasa Kajala aliyezaliwa mwaka 1985 ana umri wa miaka 36, wakati Harmonize au Harmo aliyezaliwa Machi 15, 1990 ana umri wa miaka 30.
Hata hivyo, watu wa karibu na wawili hao wamelieleza Gazeti la IJUMAA kuwa, suala la umri wa Kajala halimpi shida Harmo kwani amegusa na kunasa kwa mwanamama huyo ndiyo maana anaendelea kueneza habari za penzi lao.
Baada ya wawili hao kunaswa kwenye shoo Kanda ya Ziwa wikiendi iliyopita, Harmo anaona hakuna siri tena kama walivyokuwa wakifanya mwanzoni hivyo kifuatacho kwa sasa ni kujiachia tu.
Harmo alianza kwa kuposti kipande cha video kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram kilichomuonesha akiimba live (akapela) maneno yaliyoashiria kunasa kwenye penzi la mwanamama huyo huku akisisitiza kuwa umri ni namba tu.
Watu wake wa karibu wanadai eti kinachomdatisha zaidi Harmo ni lile umbo mtata alilonalo Kajala kwani ndiyo ugonjwa wa jamaa huyo.Mbali na kufanya akapela hiyo, Harmo pia alimposti Kajala kwenye ‘status’ yake ya WhatsApp na kusindikiza na maneno yaliyosomeka; “I love you Kajala!” kisha akasindikiza na ‘emoj’ za makopakopa akiashiria mapenzi mubashara kati yao.
Funga kazi ni juzi ambapo Harmo alikiri kuendelea kuteswa na penzi hilo la Kajala kwa kumuweka kwenye ‘profile’ yake ya ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 6.7 kisha baadaye aliiondoa.
Tetesi za Kajala kutoka kimapenzi na Harmonize zilikuja mwishini mwa mwaka jana, siku chache baada ya kuibuka madai kuwa jamaa huyo ametengana na aliyekuwa mkewe, Sarah Michelotti.
Hata hivyo, mbali na Harmonize kukiri kufa na kuoza kwa Kajala, mwanamama huyo yeye amekuwa akikana kuwa kwenye uhusiano wa mapenzi mubashara na jamaa huyo kwa maelezo kwamba ana mtu wake mwingine.
“Naomba watu watambue kuwa kila mmoja wetu yupo kwenye uhusiano wake wa kimapenzi…sasa kuendelea kutuzushia kuwa tunatoka pamoja huko ni kuharibiana maisha, kitu ambacho siyo kizuri kabisa. Waache kuharibu uhusiano wa watu,” anasema Kajala.
Stori: Memorise Richard, DAR
OPEN IN BROWSER