Waziri wa Uwekezaji Prof.Kitila Mkumbo amesema moja ya changamoto inayokwamisha uwekezaji ni kutokuwawezesha wawekezaji wanapotaka kuanza kuwekeza mara baada ya kuwahamasisha juu ya fursa zilizopo,
Akizungumza kwenye uzinduzi wa muongozo wa uwekezaji mkoa wa Singida akiwa ana muwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema tangu ateuliwe kwenye nafasi hiyo, hiyo ndiyo changamoto ambayo amekuwa akiipokea kutoka kwa wawekezaji.
“Hatua ya tatu, kuwawezesha wawekezaji na wakati mwingine hapo ndipo tunapofeli mnapiga kelele, mnapiga debe, mnahamasisha wanakuja, wakishakuja hapa tunaanza kuzungushana nenda ofisi ile, lipia kile anazungushwa miezi miwili mitatu , sita au miaka” amesema Prof.Kitila Mkumbo
Aidha amewataka kutengeneza mahusiano baina ya uwekezaji yawe ya kuaminiana na kuacha roho za kizamani na kutowanyooshea vidole wawekezaji pale wanapoanza kupata faida.
“Mahusiano yetu na wawekezaji lazima tuaminiane na tuheshiamiane huwezi kuwa unamuita mwekezaji hapa kesho amewekeza, kijana wa watu amepata pesa mambo yake yamenoga unamuita fisadi unaanza kukasirika we hela umetoa wapi ilihali amefanya biashara, kwahiyo tusichukie watu ambao wana hela na mhe rais amesema watu wenye hela tuwapende kwasababu hakuna aliyekuja kuwekeza ili abaki hivyo alivyo” amesema Prof.Kitila
Sambamba na hilo Kitila Mkumbo amewasisitiza wananchi wa Singida hususan Mkuu wa Mkoa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji katika zao la alizeti huku akisema kuwa kwasasa kipaumbele kwa alizeti hakiwezi kuwa kiwanda bali uzalishaji.