Rais Magufuli ametaka lugha ya Kiswahili kuanza kutumika katika masuala ya kimahakama na kisheria katika ngazi zote.
Dkt. Magufuli ametoa rai hiyo mapema leo akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria ambapo kaulimbinu ya mwaka huu ni, Miaka 100 ya Mahakama Kuu: Mchango wa Mahakama Katika Kujenga Nchi Inayozingatia Uhuru, Haki, Udugu, Amani na Ustawi wa Wananchi.
“Kuandika hukumu kwa Kiswahili siyo dhambi. Hii pia inatia dosari kwenye uhuru tulionao,” ameeleza Rais Dkt. Magufuli huku akimpongeza Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Zephrine Galeba kwa kutumia Kiswahili katika kutoa hukumu kwenye kesi ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi ya mwaka 2020.
Kutokana na kitendo hicho cha mfano, Rais ametangaza uamuzi wa kumpandisha cheo jaji huyo kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa.
Mbali na kuhimiza hilo, Rais ameeleza nia ya serikali kuendelea kuboresha mahakama ikiwa ni pamoja kuhakikisha uwepo wa rasilimali watu ya kutosha. Hata hivyo, amemhimiza Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma kuendelea kuwachukulia hatua watumishi wachache wanaoichafua mahakama.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika mkoani Dodoma yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, mahakama, vyama vya siasa, taasisi za kidini na kijamii.