Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amewashukia baadhi ya askari polisi wilayani Rombo kwa madai ya kujihusisha na kumiliki mitambo ya kutengeneza gongo.
Mghwira ameeleza hayo jana Jumatatu Februari 22, 2021 wakati akizungumza na wafanyabiashara pamoja na wakuu wa taasisi mbalimbali mkoani Kilimanjaro.
Amesema msako ulipofanyika wilayani humo watu kadhaa walikamatwa pamoja na mapipa ya gongo huku kukiwa na viashiria polisi kuhusika.
“Nimshukuru mkuu wa Wilaya ya Rombo (Dk Athuman Kihamia) kwa mapambano haya ya kukamata wahusika na wauzaji wa gongo, niwaonye askari polisi wote wanaojihusisha na mtandao huu wa gongo kuachana na biashara hii mara moja,” amesema Mghwira.
Amewataka watumishi wa umma kutojihusisha na biashara yoyote haramu, “wamiliki wakiwa ni askari, wananchi wakatengeneza na kuuza, biashara ya aina hii inachochea uhalifu, inaleta ubaguzi na upendeleo kati ya kampuni za pombe zinazomilikiwa na askari na zile zinazomilikiwa na raia.”
“Pombe inayomilikiwa na askari hukamatwa na kuachiwa bila adhabu, wale wasio askari huadhibiwa kwa ukali wa kupitiliza na wakati mwingine kulipa faini za wenzao matokeo yake wananchi wanaanza kutafuta askari wa kumwingiza kwenye biashara yake ili awe salama.”
“Niwatake askari wa namna hii kuachana kabisa na biashara hii haramu, ninaomba operesheni iliyofanywa na mkuu wa wilaya ya Rombo juzi itusaidie na wilaya nyingine.”
Naye Dk Kihamia amesema utengenezaji wa gongo na ulaji wa mirungi katika wilaya hiyo imekuwa tatizo kubwa akibainisha kuwa jitihada za kuwasaka wahusika zinaendelea na tayari watu 60 wameshakamatwa.
“Kwa sasa tunafanya operesheni kubwa kabisa kuhakikisha shughuli hizi za utengenezaji gongo zinakoma kabisa ikiwa ni pamoja na kung’oa mitambo yote na wahusika kupelekwa mahakamani.”
“Niwaombe wananchi wangu wa Rombo tushirikiane kuhakikisha hatutumii hizi pombe za kienyeji kwa sababu inaangamiza nguvu kazi ya Taifa hasa vijana. Tayari tumekamata mitambo 10 ya gongo na watu zaidi ya 60 tunawashikilia na shughuli hii inaendelea, nataka Wilaya hii iwe kama ilivyokuwa zamani,” amesema Dk Kihamia.