Mwanza. Serikali imesisitiza msimamo wa kutoomba wala kupokea chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia afya, Profesa Mabula Mchembe alitaja sababu mbili za Tanzania kufikia uamuzi huo.
Alitaja sababu ya kwanza kuwa ni kutojulikana ni chanjo ipi kati ya tatu zilizogunduliwa na nchi za China, Uingereza na Urusi inayofaa kwa ajili ya Watanzania.
“Hadi sasa hakuna utafiti wa kitabibu uliofanyika kubaini ni chanjo ipi inafaa kutumika kwa Watanzania,” alisema Profesa Mchembe.
Sababu nyingine kwa mujibu Profesa Mchembe ambaye ni tabibu kutaaluma ni kuwa chanjo hizo kutojulikana zinaweza kudumu kwa muda gani.
Mwananchi