Serikali Tanzania yakanusha wagonjwa wa Covid 19 kulazwa Muhimbili

 


Dar es Salaam. Katibu mkuu Wizara ya Afya nchini Tanzania, Profesa Mabula Mchembe amewataka wananchi kupuuza taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii  kuwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Mloganzila wamelazwa wagonjwa wa Covid 19.


Ameeleza hayo leo Jumanne Februari 2, 2021 alipofanya ziara katika hospitali ya Mloganzila na MNH ili kujua usahihi wa madai hayo, kusisitiza kuwa yanapaswa kupuuzwa.


"Nimepita hospitali ya Mloganzila na pia nimepita hapa Muhimbili nimekutana na wafanyakazi ili kuzungumza nao na pia  kusikia changamoto wanazopata.”


“Tumeweza kupita kwenye wodi ili kuona matatizo yaliyopo pamoja na wagonjwa. Nimejiridhisha kwamba sio kila wagonjwa waliolazwa hospitali wana ugonjwa wa corona kama ambavyo inasemekana kwenye mitandao,” amesema Profesa Mchembe.


Amesema wapo wagonjwa wenye tatizo la upungufu wa damu , wenye shida ya kupumua, waliopata ajali, kifafa, seli mundu na pumu.


“Lakini wote hawa ukijumlisha dalili zao za ugonjwa zinaweza kufanana. Wapo wanaoumwa kichwa, wenye mafua, mwingine anashindwa kupumua kutegemea na mwili wake,” amesisitiza.



Ameiasa jamii kutotumia mitandao ya kijamii kuwaogopesha wagonjwa waliopo kwenye wodi mbalimbali za hospitali hizo wakiendelea kupata matibabu na kuwataka kutambua kila binadamu ni mgonjwa mtarajiwa.


Alitumia ziara yake hiyo kuwapongeza watoa huduma ya afya nchini kwa kuendelea kuwahudumia wagonjwa kwa hali na mali licha ya changamoto wanazopitia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad