WAZIRI Mkuu wa Tanzania,Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itafuatiliwa suala la timu ya Namungo FC kushikiliwa na jeshi la Polisi nchini Angola.
Namungo FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Hemed Morocco, jana Februari 12 ilikwea pipa kuelekea nchini Angola kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya 1 de Agosto ya Angola ikiwa ni hatua ya 32 bora.
Leo imetoka ripoti kwamba timu hiyo imezuiwa kuinga nchini Angola ilipowasili Uwanja wa ndege wa Luanda kwa kile ambacho kimeelezwa kuwa wachezaji watatu wana Virusi vya Corona na kiongozi mmoja kwenye msafara huo jambo ambalo limewafanya wapewe machaguo mawili, moja kwenda karantini ama kurejea Tanzania.
Mchezo wao wa Kombe la Shirikisho unatarajiwa kuchezwa kesho, Februari 14,nchini Angola.
Akiwa bungeni, leo Februari 13, Majaliwa amesema:"Klabu ya Namungo inashikiliwa na jeshi la Angola na tunajua kwamba hizo ni sehemu za siasa za mpira. Kwa hilo ambalo limetokea tutalifuatilia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania.
"Tunawatakia kila la kheri kwenye mchezo wa kesho na tutaifuatilia ili tuhakikishe kwamba inarudi Tanzania salama,".