Dodoma. Waziri wa Kilimo wa Serikali ya Tanzania, Profesa Adolf Mkenda ametangaza kusitisha shughuli zote za maonyesho ya Nanenane zilizokuwa zifanyike mwaka huu.
Akizungumza leo Jumatano Februari 10 2021 Jijini Dodoma, Profesa Mkenda amesema fedha zote za umma bila kujali ni za wizara gani, zisitumike kwenye shughuli hizo.
“Lakini nawasiliana na wizara nyingine na wadau kwamba fedha hizo tuzielekeze katika kuendeleza shughuli za ugani,” amesema waziri huyo.
Amesema hivi karibuni walikuwa na kikao na maofisa kilimo wa mikoa, walijadiliana kwa kiasi kikubwa kuhusu changamoto ambazo baadhi zinahitaji wawezeshwe kifedha ili wazitatue.
“Tuna maofisa tumewaajiri hadi ngazi ya kata kwa ajili ya kilimo, lakini changamoto tulizozizungumza wakati ule zinahitaji na sisi kuwawezesha vilevile, kwa sababu hatuna haja ya kuweka ofisa kule lakini hatujatengeneza wao kuwasaidia watu,” amesema.
Amesema wako wakulima wanasema hawajui wanapataje huduma za ugani hivyo anawasiliana na wizara nyingine ambazo ni wadau kwenye shughuli hizo kwamba fedha yote iliyokuwa itumike kwa ajili ya shughuli za Nanenane mwaka huu ipelekwe katika shughuli za kuimarisha ugani.