Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo, ameiomba Serikali kusitisha tozo za utalii kwa Hifadhi zilizo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa(TANAPA) zilizotangazwa kuanza kutozwa Julai mwaka 2021 kutokana na sekta ya utalii nchini kuathiriwa na ugonjwa wa Corona.
Ongezeko hilo la tozo limezilenga hifadhi za Taifa nne ambazo ni Ziwa Manyara, Serengeti, Tarangire na Arusha kwa kipindi cha msimu wa juu wa utalii nchini na kuacha tozo za sasa ambazo zitaendelea kutumika kwa msimu wa chini wa utalii.
Akiuliza swali la nyongeza jana bungeni, Gambo alisema sekta ya utalii kwa Mkoa wa Arusha na nchi nzima imeathiriwa sana ambapo watu wamekosa ajira, madereva wamekosa ajira, waongoza watalii wamekosa ajira, wafanyakazi wa mahoteli wamepunguzwa kazi.
“Kwa ukanda wa Afrika Mashariki nchi nyingi zimepunguza tozo katika kipindi hichi, kwa mfano Kenya kwenye hifadhi ya Nairobi wamepunguza tozo kutoka Dola za Marekani 43,000 hadi 35,000, Rwanda wamepunguza kutoka Dola za Marekani 1500 hadi 500, Uganda wamepunguza kutoka Dola la Marekani 700 hadi 500,” alisema.
Aliomba Wizara ya Maliasili na Utalii iangalie athari za ugonjwa wa Corona kwenye masuala ya ajira na mengine.
“Wizara ina mpango gani kuipa ahueni sekta ya utalii ili kunusuru tatizo kubwa ya ajira ambayo imewaathiri wananchi wa Mkoa wa Arusha,”alihoji.
Akijibu maswali ya Mbunge huyo, Naibu Waziri wa Maliasli na Utalii, Mary Masanja, alisema wakati wafanyabiashara ya utalii wakiishinikiza Serikali kuacha tozo zikiwa za chini sana, wenyewe wamekua wakiwatoza watalii tozo za juu ambazo hawataki kuziweka wazi kwa serikali.
“Usiri wa tozo za makampuni binafsi unainyima Serikali taarifa za msingi za kuona uzito wa hoja yao, naomba kutoa rai kwamba suala la Corona lisitumike kuinyima serikali mapato ambayo yanasaidia kukuza uchumi wa nchi,”alisema.
Alisisitiza pamoja na shinikizo la kupunguza tozo, sekta binafsi haijawasilisha takwimu zozote Serikalini za kuthibitisha kuongezeka kwa idadi ya wageni waliofuta safari zao kuja nchini kutokana na ongezeko la tozo.
Alisema serikali imeongeza tozo hizo zitaendelea kutumika kwa vipindi vyote visivyo vya utalii wa juu tu na lengo la kuwa na tozo za vipindi hivyo viwili ni kuwavutia watalii wengi zaidi kutembelea vivutio hasa kipindi cha msimu wa chini wa utalii.
Aidha, alisema viwango vilivyorejewa kwa baadhi ya hifadhi vililenga kuongeza idadi ya watalii kwenye Hifadhi ambazo zimekuwa zikipata watalii wachache hasa za Kusini, Mashariki na Kaskazini-Magharibi.
“Tozo ya kuingilia Hifadhi ya Serengeti mwezi Julai mwaka huu itaongezeka kutoka Dola za Marekani 60 hadi 70, na gharama za camping zitaongezeka kwa Dola za Marekani 10 kutoka 50 hadi 60 huku kwa Hifadhi za Manyara, Tarangire na Arusha gharama za kuingia zitaongezeka kutoka Dola za Marekani 45 hadi 50 huku gharama za camping zitakuwa Dola za Marekani 60 kutoka 50,”alisema.
Hata hivyo, alisema viwango hivyo ni vidogo sana ikilinganishwa na viwango ambavyo makampuni ya utalii yanatoza kwa watalii hao.