Shahidi aieleza korti alivyomdaka askari mhalifu






Shahidi ASP Bernard Nyambalya ameieleza Mahakama ya wilaya ya Temeke kuwa aliyekuwa askari Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Shaidu Athuman alikutwa ndani ya gari walilokuwa wakitumia kwa uhalifu akiwa na sare za polisi, pingu, rungu, buti, kitambulisho cha kazi pamoja na kofia ya polisi.


Mbali na Athuman, washtakiwa wengine ambao wote walikana mashtaka, ni mfanyabiashara Shamte Jongo na Ernest Kirumbi.



Kati ya Septemba 20, 2019 maeneo ya Rangitatu, washtakiwa hao inadaiwa walimteka mfanyabiashara, Barnabas Malitu na kumwibia fedha taslimu zaidi ya Sh 10.6 milioni kabla ya kumuibia walimtishia kwa kutumia kipande cha nondo kuweza kujipatia fedha hizo.



Shahidi huyo ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kipolisi Chanika, alitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi, Karim Mushi akiongozwa na mawakili wa Serikali, Clara Charwe pamoja na Salome Assey,



Nyambalya alidai akiwa Mkuu wa Upelelezi wilaya Kipolisi Mbagala Septemba 6, 2019 mpaka Septemba 25, 2019 yalijitokeza matukio matano yanayohusiana na uhalifu wa gari nyeupe aina ya Ford Ranger ambayo ilikuwa inabandikwa namba za polisi.



Alidai kuwa walifanya uchunguzi na kubaini kuwa gari hilo ni la mtu binafsi na baadaye washtakiwa hao waliokuwa wanawavizia wafanyabiashara wa kampuni ya simu zinazotoa huduma ya pesa na wafanyabishara wakubwa wa maduka ya jumla.



“Hawa washtakiwa wakigundua ni mfanyabiashara mkubwa wanamvizia wakati akitoka dukani na kuelekea nyumbani akiwa ndani ya gari yake wanaizuia katikati ya barabara, na kwa kuwa ndani ya gari hilo anakuwamo polisi, mhusika anasimama,” alidai Nyambalya.



Alidai baadaye wanamteka mfanyabiashara na kumwigiza kwenye gari lao na kumfunga pingu huku wakimpiga na kumtishia kwa silaha na kumwibia fedha anazokuwa nazo.



Nyambalya alidai Septemba 27, 2019 alipigiwa simu na mtoa taarifa kuwa eneo la Kurasini Mji Mpya ambako kuna baa inayoitwa Contena limeonekana gari hilo.



Alidai walielekea hadi kwenye baa hiyo na walifanikiwa kuwakamata washtakiwa hao ambapo mshtakiwa Athuman alikutwa na begi jeusi lililokuwa na sare za polisi, pingu, buti, kitambulisho cha kazi pamoja na kofia ya polisi.



Shahidi huyo alidai walipopekuwa ndani gari hilo walikuta kiroba kwenye viti vya nyuma kikiwa na namba mbili za magari ya polisi, namba PT2582 na PT252 na kipande cha nondo kilichochongoka upande mmoja kinachotumika katika uvunjaji wa milango.



Pia walikuta kipande kingine cha nondo ambacho kimechongoka pande zote mbili, plasta inayotumika kuwafunga watu mdomoni na kamba ya mkonge na manila ambazo zilikuwa zinatumika kuwafunga watu mikono.



Naye shahidi ambaye ni mfanyabiashara wa jumla wa eneo Mbagala rangi tatu, Barnaba Maliti aliieleza mahakama hiyo kuwa Septemba 6, 2019 saa 12 jioni akiwa anatoka ofisini kwake na ghafla gari lenye namba za polisi PT2582 lilizuia gari lake.



Maliti alidai baada ya kuzuiwa alishuka mshtakiwa Athumani ambaye alikuwa amevaa sare za polisi akamweleza kuwa gari lake limeonekana kwenye kamera kwenye Kituo cha mafuta kilichopo Chang’ombe kwamba amejaziwa mafuta lakini dereva hakulipam hivyo anahitajika aende kituo cha polisi hicho.



Alieleza jinsi walivyomwingiza kwenye gari lao, kumfunga pingu mikononi, plasta mdomoni na kumpiga kisha kumpora zaidi ya Sh 10.6 milioni na kumtupa eneo la Kitunda Mwanagati.



Hakimu Mushi aliahirisha shauri hilo hadi Februari 15, mwaka huu kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad