Mshtakiwa wa pili katika kesi ya Uhujumu Uchumi, Shamimu Mwasha(41), anatarajia kuanza kujitetea Februari 15, 2021 katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Ufisadi.
Ni baada ya Mahakama hiyo kuwakuta na kesi ya kujibu, yeye na mume wake, Abdul Nsembo(45) maarufu Abdulkandida.
Shamimu anayemiliki Blog ya 8020 na Nsembo, wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini gramu 439.70, tukio wanalodaiwa kutenda kosa , Mei Mosi 2019, eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Shamimu atajitetea siku hiyo, baada ya mashahidi wawili wa upande wa utetezi, kumaliza kujitetea.
Mashahidi hao ni Lucas Mbaruku ambaye ni fundi CCTV na Nsembo, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo.
Uamuzi huo wa kujitetea Shamimu umetolewa leo, Februari 12, 2021 na Jaji Elinaza Luvanda, muda mfupi baada ya shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi, Mbaruku kuhojiwa na wakili wa upande wa mashtaka, Costatine Kakula kuhusiana na CCTV Camera iliyofungwa nyumbani kwa wanadoa hao.
Katika utetezi wake, Mbaruku amedai kuwa CCTV iliyofungwa ndani ya nyumba ya wanandoa hao, hajui imetengenezwa na kampuni gani nchini China.
Mbaruku, amedai kuwa kutokana na kutokujua kampuni iliyotengeneza CCTV Camera hiyo, imekuwa ni ngumu kwake kuingiza namba ya siri ili iweze kufunguka.
Shahidi huyo baada ya kumaliza kuhojiwa, Jaji Luvanda aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 15, 2021 itakapoendelea.