Shirika la Ndege la United Airlines lasitisha safari za Boeing 777 baada ya ajali

 
Shirika la ndege la United, (United Airlines) limesema linasitisha ndege zake 24 aina ya Boeing 777 baada ya moja ya ndege hizo kupata hitilafu ya injini baada ya kuruka siku ya Jumamosi.



Ndege hiyo ya Boeing 777, iliyokuwa na abiria 231 na wafanyakazi 10, ilifanikiwa kutua salama katika uwanja wa ndege wa Denver. Hakuna majeruhi walioripotiwa.

Mabaki ya ndege hiyo walionekana yamesambaa karibu na makazi ya watu.

Ikizungumzia tukio hilo, Japan imeyataka mashirika yote yanayotumia Boeing 777 zenye injini sawa ya Pratt & Whitney 4000 kuepuka kuruka.

Boeing imesema inaunga mkono uamuzi wa Japan na imependekeza kusimama kwa shughuli zote za Boeing 777 zanye injini kama hiyo wakati uchunguzi kuhusu tukio hilo ukiendelea. Watengenezaji wa aina hiyo ya ndege wamesema ndege 69 za Boeing 777 ziko kwenye matengenezo kote duniani zenye injini ya aina hiyo.

Ndege ya shirika la United, ndege nambari 328, iliyokuwa ikielekea Honolulu ilipata hitilafu kwenye injini yake ya kulia, Mamlaka ya anga( FAA) imeeleza.

Shirika limetaka uchunguzi zaidi kufanyika kwa aina ya ndege ya Boeing 777 zenye injini ya Pratt & Whitney 4000 baada ya ajali hiyo.

‘Ilikuwa ikitikisika hasa’

Mmoja wa abiria aliyekuwa ndani ya ndege hiyo ameliambia shirika la habari la AP kwamba rubani alikuwa akitoa tangazo wakati mlipuko mkubwa ulisikika.

“Ndege ilianza kuyumba yumba sana, mara ikaanza kushuka chini,” David Delucia alisema.

Aliongeza kuwa yeye na mke wake waliweka stakabadhi za utambulisho mfukoni “ili ndege ikianguka, tuweze kutambuliwa”.



Huko Japani, aina ya ndege zote za 777 zilizo na injini za Pratt & Whitney 4000 zinapaswa kuepuka kufanya safari, hii ni pamoja na kuruka na kutua.

Serikali pia imeamuru mashirika ya JAL na ANA kuacha kutumia ndege zake za Boeing 777 zenye injini ya Pratt and Whitney 4000.

Mwezi Desemba mwaka jana ndege ya JAL ililazimika kurudi Uwanja wa ndege wa Naha kwa sababu ya kuharibika kwa injini ya kushoto – ndege hiyo ilikuwa na umri sawa na ndege ya United Airlines ya miaka 26 kutoka na tukio la Jumamosi.

Mwaka 2018, injini ya kulia ya ndege ya United Airlines ilivunjika muda mfupi kabla ya kutua Honolulu. Kufuatia uchunguzi, Bodi ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri ilisema tukio hilo lilisababishwa na kuvunjika kwa mapanga ya feni.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad