China imepiga marufuku matangazo ya BBC World nchini humo, wathibiti wake wa matangazo ya televisheni na redio wamesema Alhamisi.
China imekosoa BBC kwa kutangaza taarifa za virusi vya corona na dhuluma dhidi ya kabila la walio wachache la Uighur.
BBC imesema imesikitishwa na uamuzi huo.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa mdhibiti wa vyombo vya habari Uingereza Ofcom wa kufutilia mbali leseni ya chombo cha habari cha China, Global Television Network (CGTN) kurusha matangazo yake nchini Uingereza.
Uamuzi wa Ofcom uliotolewa mapema mwezi huu baada ya kubaini kwamba leseni ya kituo cha CGTN ilikuwa inatumiwa visivyo na chombo cha habari cha Star China Media Ltd.
Wizara ya mambo ya nje imeshutumu uamuzi huo na kuuita sehemu ya kampeni kubwa ya kukandamiza vyombo vya habari nchini China.
Uhusiano kati ya China na Uingereza umezorota pakubwa siku za hivi karibuni kwasababu ya mgogoro wa Hong Kong, ambapo China ilianzisha sheria moya yenye utata baada ya kufanyika kwa maandamano makubwa eneo hilo.
Januari, Uingereza ilianzisha viza mpya ambayo inatoa fursa kwa raia milioni 5.4 wa Hong Kong haki ya kuishi Uingereza na hatimaye kupata uraia nchini humo kwasababu inaamini kwamba China inakandamiza haki na uhuru wa eneo hilo.
Na katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, China imekuwa ikifungia au kupiga marufuku vyombo vya habari vya kigeni ikiwemo kufukuza kabisa wanahabari wa magazeti matatu ya Marekani mwaka 2020.
Tovuti ya BBC na programu yake ya kwenye simu tayari vimepigwa marufuku nchini humo.
Mnamo mwezi Februari, BBC iliangazia taarifa ya mahojiano na wanawake wa Uighur waliosema kwamba wamebakwa, wamenyanyaswa kingono na kuteswa katika mpango wa utoaji tena mafunzo kwenye kambi za China mjini Xinjiang.
Wizara ya mambo ya nje ya China ilishutumu BBC kwa kutangaza "taarifa za uongo".
Mwezi uliopita, Marekani ilisema kuwa China imetekeleza mauaji ya kimbari katika hatua ya kukandamiza kabila la waliowachache la Uighur na makabila mengine ya Kiislamu.
Kulingana na makadario yaliyotolewa, zaidi ya watu milioni moja Wa Uighur na makabila mengine ya walio wachache wamekamatwa katika kambi za China.
China imekanusha madai ya Uighur wananyanyaswa.
Mwaka jana balozi wa Uingereza nchini China Liu Xiaoming alimwambia mwanahabari wa BBC Andrew Marr kwamba taarifa za msongamano kwenye kambi ni za "uongo" na kuwa Wauighur wanakabiliwa kisheria kama makabila mengine machache nchini humo.
CGTN pia ilipatikana ikikiuka kanuni za shirika la habari la Uingereza mwaka jana, kwa kutangaza kile kinachodaiwa kuwa kuungama kwa lazima kwa raia wa Uingereza Peter Humphrey.
Katika uamuzi wake, shirika la filamu la China, Televisheni na redio limesema taarifa za BBC World juu ya China zilipatikana "zinakiuka vikali" miongozo ya utangazaji, ikiwemo "hitaji la kwamba taarifa za habari zinastahili kuwa za kweli na zisizopendelea upande wowote" na wala sio "kudhuru maslahi ya taifa la China".
Inasemekana kuwa ombi la BBC la kupeperusha matangazo yake kwa mwaka mwingine halitakubalika.
Taarifa ya BBC imesema: 'Tumesikitishwa na mamlaka ya China ilivyoamua kuchukua mkondo huu. BBC ni chombo cha habari cha kimataifa chenye kuaminika zaidi duniani na hutangaza taarifa kutoka kote ulimwenguni kwa usawa, bila upendeleo wala uoga au kuunga mkono yoyote."
Kituo cha habari cha televisheni cha BBC World News ambacho hufadhiliwa kibiashara hurusha matangazo yake kwa lugha ya Kiingereza kote duniani.
Nchini China, BBC inadhibitiwa na huonekana tu katika hoteli za kimataifa na baadhi ya maeneo ya kidiplomasia, kumaanisha kwamba raia wengi wa China hawawezi kuitazma.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Dominic Raab ametaja hatua hiyo kama "isiyokubalika na inayominya uhuru wa vyombo vya habari".