Naibu waziri wa ofisi ya Rais TAMISEMI David Silinde amewaagiza kuandika maelezo ndani ya siku tatu mkuu wa shule ya sekondari ya Nachingwea Mwalimu Longinus Nambole na Afisa elimu sekondari ya kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu baada ya kushindwa kusimamia mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi shuleni hapo toka mwaka 2017 bila kukamilika huku serikali ikiwa imeshaleta fedha zote za ujenzi.
Amechukua maamuzi hayo baada ya kufanya ukaguzi katika shule na kujionea ujenzi ukiwa umesimama bila kuendelea na fedha zote milion 150 za bweni zikiwa zimemalizika na jengo moja tu ndio likiwa limekamilika na kuanza kutumika huku lingine likiwa katika hatua ya upauji hali ambayo ni tofauti na halmashauri zingine ambao wamemaliza kwa fedha hizo hizo walizopelekewa na serikali katika miradi ya lipa kwa matokeo EP4R.
“Naitaji maelezo Afisa elimu na mwalimu TAMISEMI uwe umeshayaandika ndani ya siku 3 kwanini hili jengo halijaisha kwa miaka mitatu na miezi miwili nataka mnieleze hizo gharama mlizozitumia,nimezunguka maeneo mengi watu wamejenga mabweni chini ya milioni 80 wamekamilisha na mkurugenzi unieleze jengo linaisha lini na nitakuja tena kukagua upya na hili liwefundisho afisa elimu usipotoa maelezo vizuri katika hili tutaondoka na madaraka yako” Naibu Waziri Silinde.
Kwa upande mkuu wa wilaya ya Nachingwea Hashim Komba na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri Hassan Rugwa wamesema wamepokea maelekezo ya Naibu waziri na kumwahidi mpaka kufika mwisho wa mwezi wa sita ujenzi wa mabweni katika shule hiyo na shule ya wasichana ya Nachingwea utakua umekamilika na kuanza kutumika kwa fedha za ndani za halmashauri.
Naibu Waziri Silinde yupo katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa madarasa na mabweni iliyotolewa fedha na serikali katika mradi wa lipa kwa matokeo EP4R na kutembelea wilaya ya Liwale na Nachingwea na kukagua matumizi ya fedha kutoka mapato ya ndani asilimia 40 kwa kila halmashauri zimetukikaje katika mkoa wa Lindi.