Simba vs Azam FC Kesho Kitawaka Kwa Mkapa




MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba kesho saa moja kamili usiku wanatarajiwa kuwakaribisha wapinzani wao Azam FC kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Timu hizo zitavaana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi uliosogezwa mbele ili kuipisha Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.



Katika mchezo huo, timu zote mbili zitaingia uwanjani zikiwa na makocha wapya, Simba wakiwa na Mfaransa Didier Gomes aliyechukua nafasi ya Mbelgiji Sven Vandenbroeck.

Azam FC yupo Mzambia George Lwandamina aliyemrithi Aristico Cioaba aliyesitishiwa mkataba wake kutokana na matokeo mabaya katika ligi.

 

Mchezo huo ni muhimu kwa timu hizo mbili kutokana na kuwepo kwenye mbio za ubingwa, Simba ipo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 38 ikifuatiwa na Azam 32 huku Yanga wakiongoza na 44 wakiwa na michezo miwili mbele ya Simba.

 

Pambano hilo linatarajiwa kujaa upinzani mkubwa kutokana na kila timu kufanya maboresho ya kikosi chake katika usajili wa dirisha dogo Simba ikiwa imesajili wachezaji wawili wa kimataifa watakaowatumia katika ligi ambao ni mshambuliaji Mzimbabwe Perfect Chikwende na kiungo mkabaji Mganda Taddeo Lwanga tofauti na wale watakaowatumia katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Azam wao wamesajili wachezaji watatu kipa Mganda Mathias Kigonyana na washambuliaji Mkongomani Mpiana Mozinzi na Yahya Zayd aliyesajiliwa kwa mkopo wa miezi sita akitokea Pharco ya Misri.



Akizungumzia mchezo huo, Gomes alisema kuwa anaamini utakuwa mchezo mgumu kwao, lakini muhimu kwa wachezaji wake kupambana ili kuchukua pointi tatu.Gomes alisema kuwa kikubwa wanataka kushinda michezo yote ya viporo walivyobakisha baada ya kushinda kiporo chao cha kwanza dhidi ya Dodoma Jiji FC mchezo uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Jamhiri, Dodoma uliomalizika kwa Simba kushinda mabao 2-1“Utakuwa mchezo mgumu lakini tupo tayari kupambana ni muhimu sana.

 

Tumebakisha michezo miwili mkononi katika viporo vyetu baada ya kucheza na Dodoma, tunatakiwa kushinda michezo yote ili kupunguza alama na timu iliyopo kileleni ambayo ni Yanga.“Baada ya mchezo dhidi ya Dodoma haraka tutaanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Azam ambao ni mgumu kutokana na ubora wa kikosi chao na kikubwa hivi sasa sitaangalia tunacheza vipi zaidi ni pointi tatu pekee,” alisema Gomes.



Kwa upande wa Lwandamina alisema kuwa mchezo huo unatarajiwa kujaa presha kubwa, lakini ataingia uwanjani kama mechi za kawaida.“Utakuwa mchezo mgumu ila tupo tayari kwa ajili ya ushindani na ninajua kwamba kila mmoja anafikiria juu ya presha hilo lipo wazi ikiwa unacheza na Simba ama Yanga.

 

“Ni mchezo wa kawaida hivyo tutaingia ndani ya uwanja kwa kujiamini na kujituma zaidi ili kupata ushindi,” alisema Lwandamina.Aidha, katika mchezo Azam inatajwa kumkosa beki wake wa kati Mghana Yakubu Mohamed kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano alizozipata katika michezo iliyopita.Kwa upande wa Simba wenyewe watawakosa wachezaji wao John Bocco na Erasto Nyoni wanaosumbuliwa na majeraha tangu wakiwa katika kikosi cha Stars kilichoshiriki Chan nchini Cameroon.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad