WAKATI joto la mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Al Ahly ya Misri ikizidi kupanda, benchi la ufundi la Al Ahly, limelazimika kumuondoa mshambuliaji wake wa kati, Marwan Mohsen kutokana na kupata majeraha katika mazoezi waliyofanya juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Gymkhana jijini Dar.
Al Ahly waliwasili juzi Ijumaa tayari kwa mchezo wao wa pili wa Kundi A ambao unatarajiwa kupigwa kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar.
Kwa mujibu wa Dr Ahmed Abu Abla, wamelazimika kumuondoa mshambuliaji huyo katika mazoezi yao ya kwanza ya timu hiyo nchini kutokana na kupata majeraha ya mguu.
“Tumelazimika kumuondoa. Tumeamua kufanya hivyo kwa ajili ya kumuepusha mchezaji na majeraha makubwa zaidi kwa sababu hii itasaidia kuweza kukaa sawa haraka,” alisema Dr Abla.
Marwan amefanikiwa kufunga mabao matano ndani ya mwaka huu, akifunga mabao mawili katika michuano ya Klabu Bingwa Dunia iliyomalizika hivi karibuni nchini Qatar, mawili mengine mawili kwenye Ligi Kuu ya Misri na bao moja kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ibrahim Mussa,
Dar es Salaam