Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa ambapo kwa mujibu wa taarifa ya taasisi ya utafiti ya kimataifa, Transparency International, Tanzania imepanda kutoka nafasi ya 117 mwaka 2015 hadi kufikia nafasi ya 94 kwa sasa kati ya nchi 180 duniani zilizofanyiwa utafiti.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Mbungo amesema taasisi hiyo imetoa alama 38/100 kwa nchi ya Tanzania, ambapo awali ilipata alama 30/100 na kushika nafasi ya 117 kati ya nchi 180, na sasa imepanda kwa alama 8 na kuzipita nchi 23 ndani ya miaka 5.
“Matokeo hayo ni kulingana na kiashiria cha ‘Corruption Perception Index (CPI)’ kilichoanzishwa mwaka 1995 kwa lengo la kupima hali ya rushwa katika nchi mbalimbali duniani,” amesema.
Amesema Tanzania imeshika nafasi ya pili kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikitanguliwa na Rwanda iliyopata alama 54/100. Kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania imeshika nafasi ya 7 kati ya nchi 15 ikitanguliwa na Sychelles, Botswana, Mauritius, Namibia, Afrika Kusini, na Lesotho.
Amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na dhamira ya Rais Dkt. John Magufuli baada ya kuingia madarakani mwaka 2015 kwamba aliweka mkazo mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma.
Sababu nyingine ni mabadiliko chanya ya utendaji kazi wa watumishi wa umma, na mchango wa wadau, wananchi kufichua vitendo hivyo, vyombo vya habari, na ufanisi wa TAKUKURU.
Licha ya hatua hiyo ameeleza kuwa tatizo la rushwa bado lipo hivyo ili kumaliza kabisa wananchi na wadau wametakiwa kushirikiana na TAKUKURU kuhakikisha vitendo hivyo vinafichuliwa.
Nchi za Denmark na New Zealand zimeshika nafasi ya kwanza duniani kwa kupata alama 88/100 huku Somalia na Sudan Kusini zikishika nafasi ya 180 kwa kupata alama 12/100.