Kamati ya kuchunguza utata ulioibuka kuhusu mazingira ya kifo cha aliyekuwa dereva wa lori, Abdulhman Issa imebaini kuwa dereva huyo hakupigwa na Askari wa kikosi cha usalama barabarani kama ilivyoelezwa hapo awali.
Kamati hiyo iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya RC Albert Chalamila imebaini kuwa dereva huyo amefariki akiwa njiani kupelekwa katika Hospitali ya Igawilo iliyopo jijini Mbeya.
RC Chalamila ametoa ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari leo na kueleza kuwa marehemu Issa alianza kujisikia vibaya akiwa njiani kabla ya kulazwa katika hospitali ya Mision Chimala ambapo alibainika kuwa na homa kali ya mapafu (Pneumonia).
Aidha Baada ya ripoti hiyo Chalamila ameruhusu mwili wa marehemu kuzikwa na kuagiza Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kugharamia gharama zote za mazishi kwa kushirikiana na familia ya marehemu Issa.