Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema misiba mingi iliyopo mkoani humo inatoka maeneo mengine na si kweli kuwa watu wanafariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Amesema Mkoa huo upo salama na kuwataka wananchi kupuuza taarifa hizo kwa kuwa hazina ukweli akifafanua kuwa misiba hiyo hutokea mikoa mingine na watu wanakwenda kufanya mazishi mkoani Kilimanjaro.
Mghwira ameeleza hayo leo Jumatano Februari 17, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari, “kuna taarifa zipo kwenye mitandao ya kijamii zikieleza Mkoa wa Kilimanjaro hasa mji wa Moshi kuwa na maambukizi makubwa ya corona, taarifa hii inadai uwepo mkubwa wa vifo vinavyotokana na maambukizi haya na kudai Hospitali zetu za Mawenzi na KCMC zimezidiwa kutoa huduma za msingi.”
"Taarifa hizi zinalenga kuwajengea hofu wananchi na hasa wanamichezo wanaotegemea kuja kushiriki Kilimanjaro Marathon itakayofanyika Februari 28 mwaka huu. Nitumie fursa hii kuwaambia Mkoa wa Kilimanjaro uko salama na niwatake wananchi kupuuza taarifa hizi ambazo sio za kweli.”
“Ifahamike kuwa Mkoa wetu huu una idadi kubwa ya watu waliopo ndani na nje ya Mkoa na ifahamike kuwa utaratibu uliopo ni kwamba watu wanapenda kuleta misiba nyumbani ya kila aina. Ni kawaida hapa nyumbani misiba ipo mingi wakati wote kwa sababu inaletwa lakini unashangaa wanaokuja na misiba wanasema sisi ndio tuna corona.”
Mwananchi