WABUNGE 19 wa viti maalumu wanaotokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (BAWACHA), Halima Mdee wamefika na kuendelea na kikao cha Bunge kilichoanza leo Jumanne, Februari 2, 2021 Jijini Dodoma.
Itakumbukwa Wabunge hao tayari walishavuliwa uanachama na chama chao mwishoni mwa mwaka jana kwa madai ya kukiuka utaratibu wa chama chao.
Wabunge hao ambao ni pamoja na Halima Mdee na Ester Bulaya, wametinga mjengoni wakiwa wamevalia mavazi meusi huku Mdee akiwa amevaa barakoa kwa lengo la kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona.
Hata hivyo kabla ya kuanza kikao cha Bunge, Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi na Wenye ulemavu, Jeniste Mhagama aliwaomba watoke nje kwanza.
Spika Job Ndugai ameomba wabaki nje kwanza na baada ya dua ameanza kuwaita akianza na wabunge watano wa kuteuliwa, kisha wakaingia wabunge watano wa ACT.
Mwisho waliitwa wabunge 19 wa Chadema wakiongozwa na Ester Matiko na Cesilia Pareso. Wabunge Halima Mdee na Ester Bulaya hawakuwa miongoni mwa walioingia mapema leo.